Barcelona, Hispania
Mshambuliaji mpya wa Barcelona, Robert Lewandowski ametaja tofauti iliyopo katika ligi kuu za soka Ulaya za Bundesliga ya Ujerumani na La Liga ya Hispania pamoja na kumzungumzia kocha wake wa zamani, Pep Guardiola aliyewahi kuwa naye katika klabu ya Bayern Munich ya Ujerumani.
Sambamba na hayo, Lewandowski ambaye pia ni mchezaji wa timu ya Taifa ya Poland, alizungumzia shauku yake ya kucheza soka Hispania na changamoyo iliyo mbele yake.
Kuhusu Bundesliga na La Liga, Lewandowski alisema, “Kama tutazilinganisha Bundesliga na La Liga, nafikiri Bundesliga ni ligi ambayo nguvu zinatumika zaidi katika kasi na kukimbia huku na kule hata bila ya kuwa na mpira lakini La Liga wachezaji wanatumia mbinu nyingi na kumiliki mpira zaidi, mimi niko vizuri kwa yote, na nitacheza kwa kuendana na mfumo wowote.”
Kabla ya kutua Barcelona, Lewandowski amecheza katika Bundesliga kwa miaka 12 mfululizo katika mechi takriban 400, kabla ya kutua Bayern alikuwa akiichezea Borussia Dortmund pia ya Ujerumani.
“Baada ya kuwa Munich kwa miaka mingi haikuwa rahisi kubadili klabu lakini wakati wote nimekuwa nikitaka kucheza Hispania, niko hapa kwa ajili ya kujitoa kwa ubora wangu na kuonyesha mbinu zangu na kuisaidia timu,” alisema Lewandowski.
“Nimewahi kucheza dhidi ya timu za Hispania katika Ligi ya Mabingwa na nafahamu uwezo wao, siogopi na niko tayari kwa ajili ya kuikabili changamoto,” alisema.
Akimzungumzia Guardiola, Lewandowski alimpongeza kocha huyo akisema kwamba naye amechangia mafanikio yake, “alikuwa kocha wangu kwa miaka miwili lakini hiyo miaka miwili ilikuwa kipindi kirefu cha soka kwangu kwa sababu nilijifunza na kuzungumza naye sana, Pep alinielezea mambo mengi si tu kuhusu soka, pia aliniambia kuhusu Barca na maisha yake yalivyokuwa katika klabu hii.”
“Nafikiri mambo yangu hapa Barca yatakuwa rahisi kwa sababu ya kufanya mazoezi na Pep, ni kocha mzuri na ana mambo ya kipekee katika mbinu za mchezo, nilijifunza mengi na kubadili mtazamo wangu kuhusu soka, ndani na hata nje ya uwanja,” alisema.
Kimataifa Lewandowski azichambua La Liga, Bundesliga
Lewandowski azichambua La Liga, Bundesliga
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
