Na mwandishi wetu
Uongozi wa Simba umedai kuwa licha ya kipa wao, Aishi Manula kusaini mkataba wa kuendelea kuitumikia timu hiyo lakini haikuwa rahisi kutokana na mvutano mkubwa uliokuwepo.
Asubuhi ya leo, Simba kupitia ukurasa wao wa mtandao wa kijamii wa Instagram ilieleza kuhusiana na kuingia mkataba mpya wa miaka mitatu na Manula utakaomuweka kwa Wekundu hao wa Msimbazi hadi mwaka 2025.
Awali kulikuwa na sintofahamu ya Simba kuendelea kubaki na kipa huyo baada ya taarifa mbalimbali kufafanua kuwa Manula alikuwa akiwaniwa na baadhi ya klabu za nje ya nchi huku zikiwa na ofa nono kabla ya Simba kuibuka washindi wa vita hiyo.
Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally alisema wana furaha kubwa kuona wamembakisha Manula kwa kuwa wanafahamu vita ilikuwa kubwa kutokana na timu nyingine kuitolea macho huduma yake.
“Tumefanikiwa kumuongezea mkataba mlinda mlango bora Tanzania, Aishi Manula ambaye kwa sassa ataendelea kuhudumu ndani ya klabu ya Simba kwa muda wa miaka mitatu ijayo, mkataba wake uitaisha mwaka 2025.
“Simba tuna furaha kubwa kumbakisha Manula, tunafahamu vita ilikuwa kubwa wengi walikuwa wanamtolea macho lakini mwisho wa siku amechagua kusalia Simba, kwa ubora kama wa Aishi isingekuwa busara kumpoteza na ndiyo maana mazungumzo yakawa mengi, marefu na hatimaye tumefikia makubaliano na kijana wetu,” alisema Ally.
Mbali na Manula, Simba pia hivi karibuni ilimuongezea mkataba kiungo wao mkabaji, Mzamiru Yassin, mkataba ambao utafikia ukomo mwaka 2024.
LigiKuu Simba: Haikuwa rahisi kumbakisha Manula
Simba: Haikuwa rahisi kumbakisha Manula
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
