Milan, Italia
Mshambuliaji wa Sweden, Zlatan Ibrahimovic ameongeza mkataba wa mwaka mmoja na klabu ya AC Milan, mkataba ambao utamfanya aendelee kuwa na timu hiyo akiwa na miaka 41.
Ibrahimovic kwa sasa ana miaka 40 na anatarajia kufikisha miaka 41 Oktoba mwaka huu, amesaini mkataba huo licha ya kuwa na maumivu ya goti aliyoyapata na kufanyiwa upasuaji Mei mwaka huu na kwa msimu ulioisha hivi karibuni wa 2021/22 aliifungia Milan mabao manane huku timu hiyo ikiwabwaga mahasimu wao, Inter Milan kwenye mbio za kulisaka taji la Serie A.
Uamuzi wa kusaini mkataba huo unaweza kuwashangaza wengi kutokana na umri wake na awali iliaminika kwamba maumivu ya goti yangemfanya afikie mwisho na aliwahi kunukuliwa akisema kuwa maumivu hayo yalimpa shida kiasi cha kumfanya apate tabu kulala kwa kipindi cha miezi sita.
Ibra ambaye pia amewahi kuichezea Manchester United na Paris St-Germain (PSG), alirudi AC Milan mwaka 2020 na kuisaidia timu hiyo kutwaa taji lao la kwanza la Serie A baada ya kulikosa kwa miaka mingi.
Mchezaji huyo pia alikuwapo wakati klabu hiyo ikitwaa taji hilo kwa mara ya mwisho mwaka 2011 alipojiunga nao akitokea Barcelona kwa mkopo na kucheza mechi 29 za ligi zilizozaa mabao 14.
Baada ya kuwa kwa mkopo, hatimaye alisaini mkataba wa kudumu na Milan mwishoni mwa msimu wa 2011/12 lakini aliondoka na kutua PSG katika kipindi hicho hicho.
Ibra ndiye anayeshikilia rekodi ya mabao mengi katika timu ya Taifa ya Sweden akiwa na mabao 62 katika mechi 121 ingawa si mchezaji pekee katika ligi kubwa za barani Ulaya mwenye umri mkubwa, mwingine ni Joaquin, nahodha wa Real Betis ambaye Julai 21 mwaka huu atafikisha miaka 41 na hivi karibuni amesaini mwaka mmoja na timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu Hispania maarufu La Liga.
Kimataifa Ibra, miaka 40 asaini AC Milan
Ibra, miaka 40 asaini AC Milan
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
