Paris, Ufaransa
Joyce Lomalisa Mutambala, beki mpya wa Yanga anabezwa mitandaoni kwa sababu ya jina lake kama vile jina ndilo linalocheza soka, laiti wanaombeza wangejua kwamba huko nyuma kulikuwa na Lilian pengine wasingesumbuliwa na jina hilo badala yake wangeanza kuhoji uwezo wa soka la Joyce huko alikotoka na nini Yanga itarajie.
Tukiuweka kando utani wa Yanga na Simba na kutafuta majina ya wanasoka ambayo kwa baadhi yetu yanaonekana ni ya kike, utamtaja Lilian Thuram, beki mwenye nguvu na kasi, aliyemudu vyema nafasi za kulia na katikati ambaye mbali na timu ya Taifa ya Ufaransa pia amecheza kwa mafanikio soka la kiwango cha juu katika klabu za Monaco, Parma, Juventus na Barcelona.
Lilian ambaye jina lake la kwanza ni Ruddy, jina ambalo hakuwa akilitumia kama ilivyo la Lilian, ni beki mwenye rekodi ya kuichezea mara nyingi timu ya Taifa ya Ufaransa akiwa ameichezea mara 142 kuanzia mwaka 1994 hadi 2008 alipostaafu.
Mwaka 2004 wakati wa fainali za Euro 2004 baada ya mechi ya hatua ya makundi dhidi ya England,Lilian alikuwa mchezaji wa tatu wa Ufaransa kufikisha mechi 100 akiwa na timu hiyo akitanguliwa na Marcel Desailly na Didier Deschamps kabla ya yeye kuendeleza rekodi hiyo na kufikisha mechi 142.
Akiwa na timu ya Ufaransa aliiwezesha kubeba Kombe la Dunia mwaka 1998 baada ya kuilaza mabao 3-0 Brazil iliyosheheni mastaa kina Ronaldo de Lima, Rivaldo, Leonardo, Dunga, Cafu na wengineo ambao walipewa matumaini makubwa ya kulibeba taji hilo lakini walikwama kwa Ufaransa.
Katika fainali hizo, Lilian na mabeki wenzake Bixente Lizarazu, Laurent Blanc na Marcel Desailly walitajwa kuwa ndio mhimili wa safu ya ulinzi ya timu ya Taifa ya Ufaransa wakiweka rekodi ya kufungwa mabao mawili tu katika mechi saba.

Ni kwenye fainali hizo ndipo Lilian alipofunga bao lake pekee na timu ya Ufaransa katika mechi ya nusu fainali dhidi ya Croatia, awali alilaumiwa kwa makosa yaliyoipa Croatia bao lakini akapambana na kuifungia Ufaransa bao la kusawazisha na mwishowe timu hiyo ikatoka na ushindi wa mabao 2-1 na yeye kutwajwa kuwa nyota wa mchezo kabla ya kukutana na Brazil katika mechi ya fainali.
Kabla ya fainali za Kombe la Dunia 1998, Lilian alikuwa na timu hiyo kwenye fainali za Ulaya au Euro kuanzia Euro 1996 na Euro 2000 ambazo Ufaransa ilibeba taji lakini pia alikuwa na timu hiyo kwenye Euro 2004 na Euro 2008 pamoja na fainali za Kombe la Dunia za 2002 na 2006.
Mwaka 2005, Lilian alitangaza kustaafu kuichezea timu ya Taifa ya Ufaransa lakini kocha Raymond Domenech baada ya kuona Ufaransa ikifuzu kwa tabu fainali za Kombe la Dunia 2006 zilizofanyika nchini Ujerumani aliamua kuwageukia baadhi ya mastaa watatu waliotajwa kuwa ni wa kizazi cha dhahabu na kuwashawishi kurudi kuichezea timu hiyo licha ya kutangaza kustaafu.
Lilian alikuwa mmoja wa mastaa hao pamoja na Zinedine Zidane na Claudie Makele, hapo hapo inakumbukwa kuwa ushirikiano wa Lilian na William Galls katika beki ya kati ulikuwa na maana kubwa kwa timu ya Ufaransa ambayo hatimaye ilifikia hatua ya fainali kabla ya kushindwa kutamba mbele ya Italia waliobeba kombe.
Nje ya soka, Lilian ni mwanaharakati wa kupinga ubaguzi wa rangi pengine ni kutokana na kukerwa kwake na ubaguzi uliopo kwenye soka, anaongoza taasisi inayoitwa Lilian Thuram Foundation ambayo inajihusisha na utoaji elimu kuhusu matatizo ya ubaguzi wa rangi.
Lilian pia ni mtunzi wa vitabu, tayari ameandika vitabu vinne, kimoja cha hivi karibuni kinaitwa White Thinking: How Racial Bias Is Constructed and How to Move Beyond It, ni kitabu kinachoelezea matatizo ya ubaguzi wa rangi ambacho kimeandikwa kwa lugha ya kifaransa.
Huyo ndiye Lilian, mwanasoka wa kimataifa wa Ufaransa mwenye rekodi ya kipekee duniani.
