London, England
Umri umekwenda, Cristiano Ronaldo ana miaka 37, Robert Lewandowski ana miaka 33, katika hali ya kawaida wachezaji hao wako katika umri ambao klabu inatakiwa kuachana nao au kuwaruhusu waondoke hasa wanapotaka kuondoka.
Man United haitaki kumuachia Ronaldo, Bayern Munich haitaki kumuachia Lewandowski, zile hoja zinazoaminiwa na wengi kwamba mchezaji akifikisha miaka 30 anaelekea mwisho wa ubora wake imekuwa tofauti kwa wawili hao, kwani si tu kwamba wamefikisha miaka 30 bali wamezidi umri huo na bado wanaonekana lulu, klabu zao hazitaki kuwaachia.
Wakati mbio za usajili zikiendelea barani Ulaya, Ronaldo ameshaweka wazi dhamira yake ya kutaka kuondoka Man United na Lewandowski naye ameshatangaza dhamira hiyo hiyo lakini klabu zao zimewaweka ngumu.
Lewandowski yeye ameomba aruhusiwe kuhama, akibainisha kuwa ana hamu ya kupata changamoto mpya kwingineko barani Ulaya hapo hapo akasisitiza kwamba anafahamu mabosi wake wanaweza kumzuia lakini haamini kama watafanya hivyo kwani hawana sababu ya kufanya hivyo.
Ronaldo yeye awali alihusisha mpango wa kuhama na alichokiita kuwa ni hofu ya kukosa nafasi ya kucheza chini ya kocha mpya Erik ten Haag lakini inaonekana hofu hiyo imekosa nguvu na sasa ni kama vile ameamua kuhusisha mpango wake wa kuhama na mgomo baridi.
Hadi sasa Ronaldo hajajiunga katika kambi ya timu hiyo kwa kile alichodai kwamba ana matatizo ya kifamilia, matatizo ambayo hayajawekwa wazi na tayari amekosa kuungana na wachezaji wenzake wa timu hiyo ambao jana walielekea Thailand kwa ziara ya maandalizi ya msimu wa 2022/23.
Man United wameshasema muda mrefu kwamba hawako tayari kufanya biashara ya mchezaji huyo kama ilivyo kwa Lewandowski na Bayern, awali iliaminika kwamba Ronaldo angeenda Bayern kama Lewandowski angeuzwa ili achukue nafasi yake lakini juzi ofisa mtendaji mkuu wa Bayern, Oliver Kahn naye amesema kwamba Ronaldo hayumo katika hesabu zao.
Unaweza kuwaelewa wachezaji hawa na nia zao za kutaka kuhama, Lewandowski kwa mfano amekuwa na Bayern tangu mwaka 2014, ameshinda karibu kila kitu hivyo ni sahihi kabisa kwake kwenda klabu nyingine, kimsingi Bayern imetosha anahitaji maisha mapya ya soka.
Ronaldo naye kuzikosa fainali za Ligi ya Mabingwa Ulaya ni jambo linalomuumiza kwani ni michuano ambayo imekuwa kama utambulisho wake katika soka miaka nenda miaka rudi, kuikosa kunamfanya atake kuondoka na pengine anaona kuikosa michuano hiyo ni sawa na kujimaliza lakini pia ameichezea klabu ambayo imemaliza msimu bila taji lolote ikiwa ni mara ya kwanza kwake tangu mwaka 2010.
Kwa nini klabu zao hazitaki kuwaachia wachezaji ambao umri umeenda? Ni vigumu klabu kumuachia mfungaji bora, wote umri umeenda lakini Lewandowski amemaliza msimu wa 2021/22 wa Ligi Kuu Ujerumani au Bundesliga akiwa mfungaj bora na mabao yake 35.
Kumbuka hiyo ni mara ya tano mfululizo na ni mara yake ya saba na hivyo kuifikia rekodi ya mkongwe Gerd Muller huku akivunja rekodi ya kufunga mabao mengi ya ugenini katika msimu mmoja, mabao 19, hapo hapo ana tuzo ya kiatu cha dhahabu Ulaya akiwa amebeba tuzo hiyo kwa mara ya pili mfululizo. Unaanzaje kumuacha mchezaji huyo hata kama ana miaka 33?
Ronaldo naye rekodi yake inambeba, Man United imemaliza nafasi ya sita katika Ligi Kuu England msimu wa 2021/22 lakini imemaliza msimu huo bila taji lolote wakati kwa Ronaldo amemaliza msimu huo kwa ujumla akiwa na mabao 24 na ndiye kinara wa mabao wa timu hiyo na amekuwa na mchango mkubwa kwa kila mechi, hivyo si ajabu kwa klabu yake kumzuia, unaanzaje kumuacha mfungaji bora aondoke hata kama ana miaka 37?
Misimamo ya klabu za Bayern na Man United hata hivyo inaweza ishindwe kufanya kazi hasa wachezaji hao watakapoamua kwa dhati kusimamia dhamira yao ya kutaka kuhama lakini nje ya hilo kuna ukweli kwamba mpira ni biashara.
Wakala wa Ronaldo, Jorge Mendes hivi karibuni alidaiwa kuwa na kikao na Rais wa Barcelona, Joan Laporta, kikao ambacho wanaoona mbali wanakihusisha na mipango ya kumpeleka Ronaldo katika klabu hiyo, si Barcelona tu, Mendes kuuza wachezaji ndio kazi yake na bila shaka sasa yuko sokoni akimnadi Ronaldo hivyo haitoshangaza mchezaji huyo kuondoka Man United kama ambavyo Lewandowski naye anavyoweza kuondoka Bayern.
Kimataifa Ronaldo, Lewandowski lulu Ulaya
Ronaldo, Lewandowski lulu Ulaya
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
