London, England
Katika kinachoonekana kuwa amedhamiria kuimarisha nidhamu na umoja Old Trafford, kocha mpya wa Man United, Erik ten Haag amekuja na sheria kali mpya zitakazotumika kwenye timu hiyo inayojinoa kwa msimu wa 2022/23 baada ya kuboronga msimu wa 2021/22 uliomalizika hivi karibuni.
Man United ilimaliza Ligi Kuu England msimu wa 2021/22 ikiwa nafasi ya sita na sasa bosi huyo mpya ana kazi ya kuleta mafanikio ambako moja ya mkakati wake wa kwanza katika mbio hizo ni kuimarisha nidhamu na kuleta umoja.
Kesho Ijumaa, Man United inaanza maandalizi ya msimu wa 2022/23 kwa ziara ya wiki mbili katika nchi za Thailand na Australia ambapo Ten Haag ameshawapa tahadhari wachezaji wake kuwa watajikuta katika wakati mgumu iwapo watatoka nje ya taratibu hizo.
Ten Haag ni kocha anayetambulika kwa kuwa muumini mzuri wa kusimamia nidhamu kwa wachezaji huku akiwa makini katika kufuatilia kwa karibu mambo madogo madogo ya wachezaji wake yakiwamo yale ya ndani na nje ya uwanja akiamini katika kuimarisha nidhamu kwenye kikosi.
Wachezaji hao wameambiwa kwamba mchezaji yeyote anaweza akaondolewa katika timu na Ten Haag kama akibainika kutoa siri za kwenye vyumba vya kubadilishia nguo jambo ambalo linadaiwa kuwa tatizo kubwa tangu kuondoka kwa Sir Alex Ferguson, kocha aliyejipatia mafanikio na timu hiyo akiaminika kuwa makini katika kusimamia nidhamu kwa wachezaji wake.
Ten Haag (52) pia amewaambia wachezaji wake kuwa atamsimamisha mmoja wao kama akichelewa kwenye mazoezi au vikao vya timu bila kujali hadhi aliyonayo mchezaji huyo kwenye timu na zaidi ya hilo amepiga marufuku mchezaji kunywa pombe katikati ya wiki ambayo watakuwa na mechi ili kuhakikisha wanakuwa katika ubora wao wanapokuwa uwanjani.
Kocha huyo pia ametaka wachezaji hao kupikiwa na mpishi mmoja badala ya kila mchezaji kuwa na utaratibu wa kuandaliwa chakula na mtu wake lakini pia amebadili mlo kwa wachezaji wake ambako sasa mlo utakaopatikana kwa wingi ni samaki na mboga badala ya utaratibu wa awali wa kila mchezaji kujipangia mwenyewe mlo anaotaka.
Nje ya kanuni hizo, Ten Haag amewatoa hofu wachezaji hao akiwataka kumuona ofisini kwake kama watakuwa na tatizo lolote badala ya kukimbilia kwa mawakala wao.
Kimataifa Ten Haag aja na sheria kali Man United
Ten Haag aja na sheria kali Man United
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
