Na mwandishi wetu
Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Murtaza Mangungu ameipinga kamati ya kusimamia uchaguzi na kuupinga mchakato mzima wa uchaguzi wa klabu hiyo uliotangazwa kufanyika Januari 3, mwakani.
Akizungumza Alhamisi Oktoba 29, 2026 jijini Dar es Salaam, Mangungu pia amesema klabu ya Simba kwa sasa haina mtendaji mkuu na mchakato wa kumpata mtu wa kushika nafasi hiyo unaendelea.
Katika hoja zake za kuupinga uchaguzi wa klabu hiyo, Mangungu alisema kwamba kamati iliyotangazwa kusimamia mchakato wa uchaguzi haikupitishwa kwa kuzingatia taratibu ni haramu na kamati nyingine itatangazwa.
Alisema kwamba mchakato wowote kuhusu uongozi ndani ya klabu ya Simba ni lazima uzingatie katiba ya klabu hiyo pamoja na taratibu za soka nchini Tanzania.
Katika suala la uchaguzi, Mangungu amewakumbusha wanachama wa klabu hiyo kutulia ili kuziacha mamlaka zinazohusika na usimamizi wa michezo nchini zitatue mgogoro uliopo.
Sambamba na uchaguzi, Mangungu pia alipinga mchakato uliotangazwa siku za karibuni kuhusu mabadiliko ya uwekezaji katika klabu hiyo kwa madai kwamba ni haramu na batili.
Mangungu badala yake alisema kwamba suala hilo linahitaji kutatuliwa kwa njia ya mashauriano ambayo tayari yanaendelea kati ya serikali na wadau husika.
Katika hatua nyingine Mangungu amepingana na baadhi ya wanachama na mashabiki wa klabu hiyo aliodai wanapokea fedha kwa lengo la kuchafua baadhi ya watu akidai kuwa hilo si jambo zuri.
Alisema vitendo vya aina hiyo vinaweza kuongeza mgawanyiko katika klabu ya Simba huku akiongeza bila kufafanua kuwa fedha hizo zinaongeza deni linalomhusu mwekezaji.
Kimataifa Mangungu apinga uchaguzi Simba
Mangungu apinga uchaguzi Simba
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
