Manchester, England
Kocha mkuu wa Man United, Michael Carrick na nahodha wa tiu hiyo Bruno Fernandes wameamua kufanya kikao kuweka mambo sawa kabla ya timu yao kuikabili Chelsea katika Ligi Kuu England.
Katika hali iliyoacha maswali, Fernandes alisugua benchi katika mechi dhidi ya Bournemouth iliyochezwa Jumapili iliyopita na Man United kulala kwa mabao 3-0.
Carrick inaaminika alimuweka Fernandes benchi baada ya mchezaji huyo kuziponda mbinu za Carrick timu hiyo ilipochapwa mabao 4-1 na Como katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Inadaiwa wawili hao waliamua kukaa pamoja na kufanya mazungumzo ya faragha kwenye uwanja wa mazoezi wa timu hiyo hoja kuu ikiwa ni kuweka mambo sawa baina yao.
Tayari Carrick ameshatangaza kwamba Fernandes ataendelea kuwa nahodha wa timu hiyo tofauti na matarajio ya wengi kwamba angevuliwa nafasi hiyo ingawa haikuwekwa wazi iwapo Bruno alimuomba msamaha kocha wake au la.
Hali kwa sasa si nzuri kwa kocha Carrick kutokana na matokeo mabaya ya timu hiyo ambayo inashika nafasi ya 16 katika Ligi Kuu England.
Kwa upande mwingine zipo habari kwamba ingawa matokeo ya timu hayaridhishi lakini mabosi wa Man United wanaamini kocha huyo mwenye umri wa miaka 45 anahitaji kupewa muda zaidi.
Akizungumzia nafasi ya Fernandes, Carrick alisema kwamba hakuna uamuzi tofauti uliofikiwa kuhusu nahodha wa timu na ataendelea kuwa huyo huyo.
“Sikilizeni, hakuna uamuzi utakaofanywa, atabaki kuwa Bruno (Fernandes), kila kitu tumeweka sawa katika timu na klabu ya soka, Bruno ni mchezaji muhimu katika hili kundi, amekuwa hivyo na ataendelea kuwa hivyo,” alisema Carrick.
Alisema wanachotakiwa kufanya ni kuleta mabadiliko na kufanya mambo yaende katika mwelekeo mzuri na kwa hilo Bruno amejitoa ipasavyo kufanya mambo mazuri na kwake yeye Carrick hakuna kilichobadilika.
