Na mwandishi wetu
Simba imeinyamazisha Yanga katika mechi ya Ligi Kuu NBC ikiichapa mabao 2-1 huku bao la Elly Mpanzu likibaki kuwa gumzo kwa jinsi alivyomtesa kipa wa Yanga, Djigui Diarra hadi kukaa chini.
Mpanzu alifunga bao hilo la pili dakika ya 72 kwa kuonesha ubora kwani baada ya kuinasa pasi aliwapangua mabeki wa Yanga, Bakari Mwamnyeto na Ibra Bacca ambaye aliishia kuanguka chini.
Baada ya hapo Mpanzu, akiwa na kipa Diarra, nyota huyo kutoka DR Congo hakufanya papara wakati akifunga bao hilo bali alionesha utulivu wa kiwango cha juu.
Kwanza alifanya kama anapiga shuti la mguu wa kulia badala yake akauzungusha mguu huo juu ya mpira jambo lililomfanya Diarra kujiandaa kuzuia shuti la chinichini.
Diarra akiwa katika matarajio ya kuzuia shuti la chinichini, alishtukia mpira umempita na kujaa wavuni baada ya Mpanzu kwa haraka kupiga shuti la mguu wa kushoto.
Diarra mmoja wa makipa bora kuwahi kucheza soka Tanzania alijikuta akiwa amekaa chini asiamini kilichotokea na kubaki akiwaangalia wachezaji wa Simba wakishangilia bao hilo maridadi.
Katika mechi hiyo iliyopigwa Jumamosi Oktoba 10, 2026 kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, Yanga ndio waliokuwa wa kwanza kuzichana nyavu za Simba mapema dakika ya tano.
Bao hilo la Yanga lilifungwa na nyota wao kutoka Namibia, Peter Shalulile baada ya kazi nzuri iliyofanywa na kiungo Maxi Nzengeli.

Nzengeli aliuwahi mpira uliookolewa na beki mmoja wa Simba kabla ya kuukokota na kutoa pasi ambayo, Shalulile aliitumia vyema kuipa Yanga bao hilo la kwanza.
Simba hawakusumbuliwa na bao hilo badala yake waliendelea kuonesha uhai wakimiliki vizuri mpira na kucheza pasi zilizofika mara kwa mara langoni mwa Yanga.
Yanga walipata pigo katika dakika ya 24 baada ya kuumia kwa kiungo wao kutoka Kenya, Duke Abuya ambaye alitoka na nafasi yake kuchukuliwa na Fred Ngoma.
Mabadiliko hayo ni kama vile yalizidi kuiamsha Simba ambayo hadi inakwenda mapumziko ilifanikiwa kutawala mchezo huo kwa asilimia kubwa huku Yanga wakiwa na kazi ya kuokoa mashambulizi.
Dakika ya 68 juhudi za Simba zilizaa matunda walipopata bao la kwanza lililofungwa na Neo Maema, bao ambalo ni kama vile liliwatia moto wachezaji wa timu hiyo na hatimaye kuandika bao la pili lililofungwa na Mpanzu.
Ushindi wa mechi hiyo maarufu Dar Derby, umewapa amani mashabiki wa Simba ambao mara ya mwisho kuifunga Yanga ilikuwa mwaka 2023 waliposhinda mabao 2-0, mabao yaliyofungwa na Kibu Denis na Henock Inonga.
Mara ya mwisho timu hizo zilikutana Agosti mwaka huu kwenye mechi ya Ngao ya Jamii iliyochezwa kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar na Yanga kutoka uwanjani na ushindi wa bao 1-0.
