Berlin, Ujerumani
Habari zilizovuma wiki kadhaa zikimhusisha nyota wa Man United, Cristiano Ronaldo kujiunga na klabu ya Bayern Munich huenda zikakoma baada ya kigogo wa klabu hiyo kusema kwamba hawana mpango wa kumsajili mchezaji huyo.
Ronaldo amekuwa gumzo hivi karibuni hasa baada ya kudai kwamba anataka kuondoka Man United huku Bayern ikiwa moja ya klabu iliyotajwa kutaka kumsajili, habari ambayo ilikolezwa na habari nyingine iliyodai kwamba Ronaldo angeenda Bayern kuziba pengo la mshambuliaji mkongwe wa timu hiyo, Roberto Lewandowski ambaye naye amewahi kusema anataka kuihama timu hiyo.
Oliver Kahn ambaye ndiye mtendaji mkuu wa Bayern amesema kwamba Ronaldo kwa sasa hafai katika mipango ya klabu hiyo na hivyo hawana mpango wowote wa kutaka kumsajili mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 37 ambaye mbali na Bayern inadaiwa pia anatakiwa na klabu za Chelsea na Napoli.
“Na ingawa naweza kumuweka Cristiano Ronaldo katika viwango vya juu, ni mmoja wa wachezaji wakubwa lakini uhamisho wake hauendani na falsala zetu,” alisema Kahn katika mazungumzo yake na gazeti moja la Ujerumani.
Bayern pia inadaiwa kutokuwa tayari kumuuza Lewandowski licha ya mchezaji huyo kusisitiza kwamba anataka changamoto nyingine Ulaya na tayari Barcelona imewasilisha kwa mara ya tatu ofa ya Euro milioni 40 kumtaka mchezaji huyo lakini Kahn amewaambia kwamba nyota huyo kutoka Poland hauzwi hali ambayo inazidi kufifisha uwezekano wowote wa Ronaldo kwenda Bayern.
Ni hivyo hivyo kwa kocha mpya wa Man United, Erik ten Haag ambaye licha ya Ronaldo kudai anataka kuhama lakini naye amesema kwamba mchezaji huyo aliyefunga mabao 24 msimu uliopita hauzwi na anataka we sehemu ya kikosi chake katika msimu wa 2022/23.
