Paris, Ufaransa
Paris, Ufaransa
Sasa ni rasmi kocha Mauricio Pochettino ameondoka katika klabu ya Paris St-Germain (PSG) ya Ufaransa na hivyo kuhitimisha miezi yake 18 na klabu hiyo huku kocha wa zamani wa Nice, Christophe Galtier akitarajiwa kuchukua nafasi hiyo.
Tangu mwezi uliopita, Pochettino amekuwa akidaiwa kutokuwa na nafasi tena katika klabu hiyo huku aliyekuwa kocha wa Real Madrid, Zinedine Zidane akihusishwa kuchukua nafasi hiyo kabla mwenyewe hajaibuka na kusema hakuwa tayari kwa kazi hiyo.
Pochettino (50) kocha wa zamani wa Tottenham hatimaye amehitimisha kile ambacho wachambuzi wengi wa soka walikitabiri muda mrefu huku baadhi yao wakiamini kwamba kilichobaki kwa kocha huyo ilikuwa ni muda tu wa kuachwa na kutangazwa mrithi wake.
Kocha huyo alionekana kutokidhi matarajio ya klabu hiyo kwani licha ya PSG kutwaa taji la Ligi Kuu Ufaransa au Ligi 1 ambalo ni taji la kwanza kubwa kwa kocha huyo, kutolewa kwake mapema kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya (hatua ya 16 bora) na Real Madrid kulionekana kuwakera mabosi wa klabu hiyo mashabiki kwani msimu mmoja kabla pia walitolewa lakini katika hatua ya nusu fainali.
Taarifa ya PSG kuachana na kocha huyo ilieleza, “Paris Saint-Germain inathibitisha kwamba Mauricio Pochettino amefikia tamati ya majukumu yake katika klabu, tunapenda kumshukuru yeye na wasaidizi wake kwa kazi waliyoifanya na tunawatakia kila la kheri kwa mambo yao yajayo.”
Pochettino ambaye pia ni beki wa zamani wa timu ya Taifa ya Argentina, kabla ya PSG aliwahi kuzinoa timu za Espanyol, Southampton na Tottenham alikojipatia mafanikio kabla ya kutua PSG miezi 18 iliyopita.
