London, England
Matumaini ya klabu ya Manchester United kumsajili beki wa kushoto wa Feyenoord, Tyrell Malacia yamefika pazuri baada ya makubaliano kufikiwa huku klabu ya Lyon ikidaiwa kuvurugiwa mipango yao ya kumpata mchezaji huyo.
Uhamisho wa Malacia ambaye ada yake inatajwa kufikia Pauni 13 milioni uliingia utata uliotokana na wakala wa mchezaji huyo ambaye inadaiwa ndiye huyo huyo anayesimamia masuala ya usajili ya Frenkie De Jong, mchezaji mwingine ambaye pia Man United inawania kumsajili.
Malacia ambaye ndio kwanza ana miaka 22 na amewahi kuichezea mara tano timu ya Taifa ya Uholanzi alitaka mmoja wa wanafamilia wake kusimamia mazungumzo ya mkataba wake suala ambalo tayari pande mbili zinadaiwa kumalizana huku kukiwa na habari kwamba Lyon ya Ufaransa nayo ilishaanza mipango ya awali ya kumsajili mchezaji huyo na mipango yao ilikuwa ikienda vizuri.
Malacia alikuwa kivutio katika kikosi cha Feyenoord ambacho kilishindwa kutamba mbele ya Roma katika mechi ya fainali ya Europa Conference Ligi na katika kipindi hicho alikuwa akiwindwa na Lyon ya Ufaransa lakini ni Man United ambao sasa wanaelekea kumsajili.
Habari zaidi kutoka Lyon zinadai kuwa klabu hiyo haijafurahishwa kwa namna ambavyo Man United imemsajili Malacia kama vile kwa kufanya umafia na kuvuruga mipango yao kwani mambo yalikuwa yakienda vizuri na mchezaji huyo alikuwa njiani kutua Lyon kabla ya Man United kuingilia kati.
Wachezaji wa Man United wanatarajiwa kuingia kambini wiki ijayo kujiandaa na maandalizi ya msimu mpya wa 2022/23 kwa safari ya Bangkok Julai 8 ambako wakiwa huko watacheza na Liverpool ikiwa ni sehemu ya maandalizi yao ya msimu huo mpya.
Baada ya Malacia, mabosi Man United wanaendelea na mazungumzo ya usajili wa De Jong ambaye klabu yake ya Barcelona imeonekana kusita kumtoa kirahisi huku bosi mpya wa Man United, Erik Ten Hag akidaiwa kumtaka mchezaji huyo katika kikosi chake.
Kimataifa Beki Feyenoord aelekea Man Utd
Beki Feyenoord aelekea Man Utd
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
