Cairo, Misri
Baada ya kupambana kwenye fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) wachezaji mastaa wa Afrika, Mohamed Salah wa Misri na Sadio Mane wa Senegal sasa watachuana katika kinyang’anyiro cha kuwania tuzo ya mwanasoka bora wa Afrika kwa msimu wa 2021/22.
Wachezaji hao ambao wamekuwa pamoja katika klabu ya Liverpool msimu wa 2021/22 ni miongoni mwa wachezaji 30 walio kwenye orodha ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) wanaowania tuzo hiyo kwa upande wa wanasoka wanaume.
Baada ya kuwa pamoja Liverpool, Mane tayari amejiunga na Bayern Munich ya Ujerumani wakati hatma ya Salah bado haijajulikana kama atabaki Liverpool au ataihama timu hiyo huku akihusishwa na mipango ya kujiunga na klabu mbalimbali za Ulaya.
Wachezaji hao pia waliiwezesha Liverpool kutwaa taji la FA na la Ligi lakini wakakwama kuiwezesha kulibeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya mbele ya Real Madrid walipochapwa bao 1-0 katika mechi ya fainali iliyopigwa jijini Paris Mei 28 mwaka huu.
Katika fainali za Afcon Februari mwaka huu timu zao zilikutana lakini alikuwa ni Mane aliyeibuka kinara baada ya Senegal kuibwaga Misri na hatimaye kulibeba taji na sasa mashabiki wanasubiri kuona nani kati yao atatwaa tuzo ya mwanasoka bora Afrika.
Mwaka 2019, Mane ndiye aliyetwaa tuzo hiyo kwa upande wa wanaume wakati, Asisat Oshoala wa Nigeria aliibeba kwa upande wa wanawake na baada ya hapo tuzo hizo hazikutolewa tena kutokana na janga la corona ingawa Salah aliwahi kuibeba mara mbili hapo kabla na amemaliza msimu uliopita katika Ligi Kuu England akiwa kinara wa mabao akiwa amefungana kwa mabao na straika wa Tottenham Hotspur, Son Heung-min.
Wachezaji wengine wanaowania tuzo hiyo ni Riyad Mahrez wa Algeria anayekipiga katika klabu ya Man City ambao ndio vinara wa Ligi Kuu England msimu wa 2021/22 huku pia wakiwamo mastaa wa Gambia, Musa Barrow na Youssouf M’Changama wa Comoro. Wengine ni kipa wa Chelsea, Edouard Mendy, Kalidou Koulibaly, Saliou Ciss na Nampalys Mendy ambao wote wanatokea Senegal.
Katika orodha hiyo ambayo inahusisha mafanikio ya wachezaji hao kwa kipindi cha Septemba hadi Juni pia wamo Franck Kessie wa Ivory Coast anayekipiga AC Milan.
Orodha kamili ya wachezaji hao ni kama ifuatavyo…
Sadio Mane (Senegal)
Edouard Mendy (Senegal)
Kalidou Koulibaly (Senegal)
Nampalys Mendy (Senegal)
Saliou Ciss (Senegal)
Riyad Mahrez (Algeria)
Mohamed Salah (Misri)
Mohamed Abdelmonem (Misri)
Mohamed Elneny (Misri)
Mohamed El Shenawy (Misri)
Bertrand Traore (Burkina Faso)
Blati Toure (Burkina Faso)
Edmund Tapsoba (Burkina Faso)
Andre-Frank Zambo (Cameroon)
Karl Toko Ekambi (Cameroon)
Vincent Aboubakar (Cameroon)
Ali Maaloul (Tunisia)
Moses Simon (Nigeria)
Youssouf M’Changama (Comoro)
Franck Kessie (Ivory Coast)
Sebastien Haller (Ivory Coast)
Musa Barrow (Gambia)
Naby Keita (Guinea)
Achraf Hakimi (Morocco)
Sofiane Boufal (Morocco)
Yahya Jabrane (Morocco)
Yassine Bounou (Morocco)
Aliou Dieng (Mali)
Yves Bissouma (Mali)
Hamari Traore (Mali)
