New York, Marekani
New York, Marekani
Miaka 13 imetimia tangu mfalme wa muziki wa pop duniani, Michael Jackson aage dunia, kwa sasa amelala pale Memorial Park mjini California huku kazi zake za muziki zikiendelea kuzalisha fedha za maana kama vile bado yu hai.
Watoto waliozaliwa wakati dunia ikiwa katika msiba huo au waliozaliwa mwaka mmoja au miwili baadaye, baadhi yao tayari wanamjua Michael Jackson na wanazipenda kazi zake ikiwamo kuziimba.
Ilikuwa Juni 25, 2009, dunia iliposhitushwa na kifo cha Michael Jackson, msiba uliotokea wakati ambao wapenzi wa muziki duniani kote walikuwa wakisubiri kwa hamu kujua nini atakifanya katika onyesho lake la This Is It lililopangwa kufanyika Julai 13, 2009 na Machi 6, 2010 katika 02 Arena jijini London.
Shauku kubwa ya onyesho la This Is It pia ilichangiwa na ukimya wa muda mrefu wa msanii huyo lakini pia wengi walitaka kujua Michael Jackson akiwa na miaka 50 angemudu kucheza kwa kasi, nguvu na kwa muda mrefu kama ilivyokuwa alipokuwa na miaka 20 na 30 wakati huo akiiteka dunia na vibao vyake moto kama Thriller, Bad, Dangerous, Black or White, Remember the Time na vinginevyo?
Ni wakati ambao miondoko iliyoitwa ‘moon walk’ iliwafanya baadhi ya mashabiki wa muziki kuamini kama ni tukio la kweli kutokana na video zilizotapakaa duniani kote zikimuonyesha Michael Jackson mwenye uwezo wa ajabu kuimba na kucheza.
Hapo hapo akakumbukwa kwa mafanikio ya miaka ya 1990 pale aliposaini mkataba wa Dola 65 milioni na kampuni ya Sony wakati huo huo akitamba na albamu yake ya nane ya Dangerous inayotajwa kuuza mamilioni ya nakala duniani kote.
Ni kipindi ambacho vibao vya Black or White na Remember the Time vilizidi kuupaisha umaarufu wa Michael Jackson duniani lakini wakati huo huo akaonekana kwenye onyesho la tuzo za muziki za Soul Train akiimba kibao cha Remember the Time muda mrefu akiwa amekaa kwa alichodai kuwa aliumia kiwiko cha mguu mara mbili wakati akifanya mazoezi kwa ajiliya onyesho hilo.
Wakati huo ukimtaja Michael Jackson ulikuwa unazungumzia mwanamuziki ambaye tafiti mbalimbali zilionyesha kwamba alifanikiwa kuuza nakala zaidi ya milioni 400 duniani kote na kumfanya awe mwanamuziki mwenye rekodi ya kipekee ya mauzo duniani.
Mafanikio hayo kwa ujumla yalimuwezesha kutwaa tuzo mbalimbali zikiwamo tuzo za Guinness World Records, tuzo 13 za Grammy, tuzo ya msanii wa karne, msanii bora wa miaka ya 1980, msanii bora wa kiume wa milenia na nyinginezo nyingi.
Ni mafanikio ambayo yaliakisi jina la Mfalme wa Pop kwa kuwa ndiye aliyetajwa kuibadili sanaa ya muziki huo kwa umahiri na ubora kupitia video ambazo ni kama vile zilitoa fursa kwa pop ya kisasa ambayo imekuwa kimbilio la wanamuziki wengi.
Zama za tuzo na mafanikio hayo pia ziliandamana na kipindi cha ukimya kwenye burudani, Michael Jackson akawa mtu wa kwenye vyombo vya habari akisakamwa na kashfa za udhalilishaji watoto na baadaye zikaanza kujengeka fikra kwamba alikuwa amefika mwisho, umri ulianza kumtupa mkono na alionekana mtu wa kula pensheni au matunda ya mafanikio yake katika muziki kabla ya kuja kwa habari ya onyesho la This Is It.
Shauku waliyokuwa nayo mashabiki kutaka kumuona Michael Jackson akitumbuiza katika This Is It, pia ilikuwa na mashali na mojawapo ni je This Is It ingeweza kukata kiu yao kwa kuwakumbusha zama hizo alipoishika dunia? Angekuwa na nguvu na uwezo wa kucheza? Bahati mbaya siku 18 kabla ya onyesho la kwanza, Michael Jackson akafariki dunia.
Hadithi ya Michael Jackson ikaishia hapo, hadithi iliyofuata ni ya fedha lukuki ambazo zinaingia kwa jina la msanii huyo kupitia hakimiliki kwenye mikataba mbalimbali, licha ya kuwa yupo kaburini kwa miaka 13 sasa.
Mwaka 2020, jarida maarufu la Forbes lilimtaja kuwa ni msanii maarufu marehemu ambaye amekuwa akiingiza fedha nyingi kila mwaka tangu afariki dunia isipokuwa mwaka 2012 tu. Kwa mfano miaka minane baada ya kifo chake, Forbes walionyesha kuwa msanii huyo pato lake lilifikia zaidi ya dola milioni 400.
Na huenda akaendelea kuingiza fedha kwa kuwa tayari watoto wa kizazi kipya katika zama ambazo wamemsikia Michael Jackson akiwa amekufa wameanza kuzipenda kazi zake na hivyo haitoshangaza miaka mingine ijayo Forbes wakaja na hadithi nyingine ya pesa ndefu anazoingiza Michael Jackson akiwa kaburini.
Hadi anafariki dunia, mbali na mafanikio Michael Jackson anabaki kuwa msanii au mtu maarufu aliyeishi maisha ya ajabu, amewahi kufunga ndoa mara mbili, na zote zikavunjika katika namna ya ajabu ajabu, ndoa ya kwanza na Lisa Marie Presley mwaka 1994 na kuvunjika mwaka 1996, mwaka huo huo akafunga ndoa na Debbie Rowe lakini wakaachana miaka mitatu baadaye.
Anatajwa kuwa ni baba wa watoto watatu lakini kwa muda mrefu kumekuwa na shaka juu ya ukweli kama watoto hao ni wake au la ingawa hali kidogo ilibadilika wakati wa msiba wake, mmoja wa watoto hao alipojitokeza na kuzungumza mbele ya halaiki kwani wakati wa uhai wake, Michael Jackson hakutaka watoto hao wajulikane.
Akiwa ghorofani kwenye hoteli moja nchini Ujerumani Michael Jackson aliwahi kumtoa mtoto wake mmoja na kuwaonyesha mashabiki wake waliojazana nje ya hoteli hiyo lakini alifanya hivyo katika namna ya kumfichaficha.
