Na mwandishi wetu
Simba leo imemuaga vizuri nyota wake Larry Bwalya kwa ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya KMC katika mechi ya Ligi Kuu ya NBC iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
KMC ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao hilo mfungaji akiwa Hassan Kabunda dakika nne kabla timu hazijaenda mapumziko bao ambalo lilianza kuibua hisia kwamba huenda mambo yangewaribikia Simba katika mechi hiyo ambayo pia waliifanya kama ya kumuaga Bwalya.
Mambo yalianza kuwaharibikia KMC kipindi cha pili baada ya Kibu Dennis kuisawazishia Simba bao katika dakika ya 52 akiitumia krosi ya Pape Sakho, bao ambalo ni kama liliamsha ari ya Simba kwani dakika 11 baadaye Sakho akaifungia Simba bao la pili.
Kabla KMC hawajatulia walishitushwa na bao lingine dakika tatu baadaye safari hii likifungwa na beki kisiki wa timu hiyo, Henock Inonga akimalizia kwa kichwa krosi ya Sakho na hivyo kuifanya Simba ifikishe pointi 57 katika msimamo wa ligi huku ikimuaga vyema Bwalya ambaye anaelekea nchini Afrika Kusini kucheza soka katika klabu ya Amazulu FC.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyochezwa leo, Ruvu Shooting wakiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Mabatini, Pwani walishindwa kuitumia vyema neema ya kuwa nyumbani baada ya kujikuta wakilala kwa bao 1-0 mbele ya Mbeya City.
Soka Simba yaipiga KMC Bwalya akiagwa
Simba yaipiga KMC Bwalya akiagwa
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
