Moscow, Urusi
Nahodha wa zamani wa timu ya Taifa ya Urusi, Igor Denisov ameibuka hadharani kupinga vita na uvamizi wa kijeshi uliofanywa na nchi yake dhidi ya Ukraine.
Denisov anakuwa mmoja wa wanamichezo wachache waliopata mafanikio kuizungumzia nchi yake katika namna ya kupinga vita jambo ambalo linaonekana kuwa ni hatari na linaweza kumfanya afungwe, kushitakiwa au hata kuuliwa.
Mchezaji huyo aliyekuwa akicheza nafasi ya kiungo, aliichezea timu ya Taifa ya Urusi mara 54 kati ya mwaka 2008 hadi 2016, alisikika kupitia mitandao ya kijamii akiuita uvamizi wa nchi yake dhidi ya Ukraine kuwa ni maafa na uharamia.
“Labda wanaweza kunifunga jela au hata kuniua kwa maneno haya lakini nayasema kama yalivyo,” alisema Denisov katika hali ya kujiamini.
Ukiachana na timu ya Taifa, Denisov amezichezea klabu maarufu nchini Urusi za Zenit St Petersburg na Lokomotiv Moscow ambapo akiwa Zenit amecheza zaidi ya mechi 300 kabla ya kuhamia Lokomotiv alikostaafia, alisema kwamba anaipenda Urusi na hataki kuihama nchi hiyo.
Katika kufikisha ujumbe wake huo, Denisov mwenye umri wa miaka 38 sasa, amemwandikia barua Rais Vladimir Putin wa Urusi kuelezea anavyopinga uvamizi huo uliofanyika kwa mara ya kwanza Februari mwaka huu.
“Mimi ni mtu ninayejivunia, nimefanya hivi ikiwa ni baada ya siku tatu au nne kupita, nimefikia hatua ya kumwambia kwamba niko tayari kumpigia magoti ili tu aachane na vita,” alieleza Denisov ambaye sasa anakuwa miongoni mwa watu maafrufu wachache wanaoishi Urusi ambao wamejitokeza hadharani kupinga uvamizi wa nchi yao dhidi ya Ukraine.
Mwanamichezo mwingine aliyejitokeza kupinga vita ni Nadya Karpova, mshambuliaji wa timu ya Taifa ya wanawake ya Urusi ingawa kwa sasa anaishi Hispania.
Vyombo vya habari nchini Urusi navyo inadaiwa vimepigwa marufu kutumia neno vita au uvamizi katika kuelezea kinachoendelea kati ya Ukraine na Urusi.
Kimataifa Mchezaji Urusi apinga vita Ukraine
Mchezaji Urusi apinga vita Ukraine
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
