Hatimaye Pogba arudi Juventus
London, England
Kiungo Paul Pogba hatimaye amekamilisha usajili wa kurudi katika klabu yake ya zamani ya Juventus ya Italia akiwa mchezaji huru baada ya kuachana na Manchester United.
Uhamisho wa mchezaji huyo baada ya kuachana na Man United umekuwa moja ya mijadala mikubwa ya uhamisho wa wanasoka barani Ulaya huku Pogba mwenye umri wa miaka 29 akishindwa kueleweka anaelekea wapi baada ya kuaga rasmi Man United.
Awali mchezaji huyo aliwahi kuhusishwa na mipango ya kuhamia kwa majirani wa Man United, Man City lakini akanusha habari hizo akisisitiza kwamba asingekuwa tayari kuondoka Man United na kwenda kwa majirani na mahasimu wao, Man City.
Pogba alisajiliwa Man United mara ya kwanza mwaka 2009 akiwa kijana mdogo na mwaka 2012 akahamia Juventus kabla ya kurudi United mwaka 2016 katika usajili uliokuwa gumzo huku akiaminika angekuwa msaada katika kubadili mambo katika timu hiyo na kuifanya iwe yenye mafanikio makubwa.
Uhamisho huo wa mwaka 2016 licha ya kuwa tukio kubwa na lililopambwa lakini mbele ya wengi matokeo yamekuwa tofauti na matarajio na kiujumla Mfaransa huyo anaonekana kama aliyefeli kwenye kikosi cha Man United.
Pogba katika msimu wake wa mwisho alijikuta akipata tabu mbele ya mashabiki wa Man United ambao waliona kama vile hakuwa na msaada mkubwa kwenye timu yao.
Akiwa Juventus kwa miaka minne Pogba alipata mafanikio kwa kuiwezesha timu hiyo kutwaa mataji manne ya ligi ya Serie A na mawili ya Coppa Italia na sasa anarudi katika kikosi hicho kinachonolewa na kocha Massimiliano Allegri na mtihani wao wa kwanza utakuwa ni taji la Serie A ambalo timu hiyo ililibeba mara ya mwisho mwaka 2020.
