London, England
Straika Darwin Nunez sasa mali ya Liverpool baada ya klabu hiyo kukubaliana na Benfica kumsajili mchezaji huyo kwa ada ya Pauni 64 milioni na mkataba wa miaka sita.
Usajili huo umekamilika baada ya vuta vikuvute ya siku kadhaa huku ikidaiwa kwamba Liverpool licha ya kumtaka nyota huyo wa Uruguay mwenye umri wa miaka 22 lakini walikuwa wagumu katika masuala ya fedha kabla ya kufikia muafaka leo hii.
Mashabiki wa Liverpool wanamkumbuka mchezaji huyo kwa mara ya mwisho akiiwakilisha Benfica dhidi ya Liverpool kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ambapo alifunga katika mechi ya kwanza ambayo Liverpool ilishinda kwa mabao 3-1 na akafunga tena katika mechi ya pili ambayo timu hizo zilitoka sare ya mabao 3-3.
Nunez mwenye rekodi ya kufunga mabao 34 katika mechi 41 za michuano tofauti ya msimu uliopita akiwa na Benfica, pia alikuwa akiwaniwa na Manchester United lakini tatizo likawa hilo hilo la malipo kwani Benfica ambao walimnunua kutoka klabu ya Almeria ya Hispania mwaka 2020 kwa ada ya Pauni 20.5 milioni hawakuwa tayari kumtoa kirahisirahisi.
Hadi sasa, Nunez ameichezea timu ya Taifa ya Uruguay mara 11 na katika mechi za ligi pekee kaifungia Benfica mabao 26 katika mechi 28 za msimu wa 2021/22 ambapo kati ya mabao hayo, 25 ameyafunga katika mechi 24 alizoichezea timu hiyo kuanzia kipindi cha kwanza.
Liverpool pia tayari imemsajili nyota wa Ureno, Fabio Carvalho mwenye umri wa miaka 19 ambaye alikuwa akiichezea Fulham na anatarajia kujiunga rasmi na timu hiyo Julai mosi mwaka huu.
Haijajulikana baada ya Nunez na Carvalho, Liverpool itamsajili nani hasa baada ya kukataa kumuuza nyota wake Sadio Mane kwa ada ya Pauni 30 milioni ambazo Bayern Munich ya Ujerumani walikuwa tayari kutoa huku majaliwa ya mchezaji huyo kwa msimu ujao yakiwa njia panda kama ilivyo kwa mkali wao wa mabao, Mohamed Salah ambao wote baada ya msimu ujao watakuwa wachezaji huru.
Kimataifa Nunez sasa mali ya Liverpool
Nunez sasa mali ya Liverpool
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
