London, England
Aston Villa imefuzu kucheza fainali za Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya kwanza baada ya Tottenham Hotspur kulala kwa mabao 2-0 mbele ya Man City katika mechi ya Ligi Kuu England (EPL) iliyopigwa jana Jumanne.
Matokeo ya mechi ya Man City na Spurs yameifanya Villa kushika nafasi ya nne ikiizidi Spurs kwa ponti tano ambazo timu hiyo haiwezi kuzifikia katika mechi moja iliyobaki kabla ya kufungwa kwa pazia la EPL msimu huu wa 2023-24.
Spurs na Villa ambazo zimetanguliwa na Arsenal, Man City na Liverpool katika nafasi tatu za juu, zimekuwa zikichuana kuwania nafasi ya nne ili kushiriki ligi hiyo kubwa lakini hatimaye ni Villa iliyoshinda vita hiyo.
Tangu michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ibadilishwe kutoka Kombe la Klabu Ulaya msimu wa 1991-92, Villa haikuwahi kushiriki michuano hiyo na hivyo kufanikiwa kufuzu msimu huu chini ya kocha Unai Emery (pichani) ni historia mpya kwa klabu hiyo.
Mara ya mwisho Villa kucheza michuano hiyo wakati huo ikiitwa Kombe la Klabu Ulaya, ilikuwa msimu wa 1982-83 takriban miaka 41 iliyopita na msimu mmoja kabla timu hiyo ilifanikiwa kulibeba taji hilo.
Mara baada ya matokeo ya mechi ya Spurs na Man City kujulikana mashabiki wa Villa walianza kushangilia timu yao kufuzu ligi ya mabingwa huku wakimpongeza Emery kwa mafanikio hayo.
“Ni siku ya kipekee, hii ni ndoto yetu tulianza msimu ili tufikie hatua hii, tumekuwa na janga la wachezaji majeruhi lakini timu hii wakati wote ilikuwa makini, ni jambo zuri, kucheza ligi ya mabingwa ni kitu bora,” alisema Emery.
Emery kocha wa zamani wa Arsenal, alianza kuinoa Villa Oktoba 2022 wakati huo timu ikiwa nafasi ya 14 kwenye EPL ikihaha kujinasua mkiani lakini taratibu alifanikiwa kubadili upepe na hatimaye timu hiyo imefuzu ligi ya mabingwa.
Naye beki wa timu hiyo, Lucas Digne alisema awali hakuna aliyetarajia timu yao kufikia hatua hiyo lakini walijiamini na kuamini katika ndoto yao na hatimaye kufanikisha jambo gumu na kupata mafanikio ya kipekee.
Kimataifa Villa yafuzu ligi ya mabingwa mara ya kwanza
Villa yafuzu ligi ya mabingwa mara ya kwanza
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
