Bellinzona, Uswisi
Rais wa zamani wa Fifa, Sepp Blatter amekana kuidhinisha malipo ya kifisadi kwa mshirika wake Michel Platini ambaye ni rais wa zamani wa Uefa.
Blatter ambaye ametoa hoja hiyo leo katika mahakama moja ya jinai nchini Uswisi baada ya kushindwa kufanya hivyo jana kutokana na kuugua ghafla, alisema malipo aliyoidhinisha kwa Platini yalikuwa ni makubaliano ya watu wawili walioaminiana.
Alisema kwamba alimuomba Platini awe mshauri wake mara tu baada ya kuchaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa rais wa Fifa mwaka 1998.
Blatter aliiambia mahakama hiyo kwamba Platini alitaka alipwe Pauni 816,030 kwa mwaka lakini Blatter akamwambia kwamba Fifa haiwezi kumudu mshahara huo na badala yake wakakubaliana kumlipa Pauni 244,809 kwa mwaka na malipo mengine ya jumla kulipwa siku nyingine.
“Nilijua tulipoanza na Michel Platini hayo hayakuwa malipo yote, tungeangalia mengine hapo baadaye,” alisema Blatter akizungumzia malipo ya Platini kwa kazi aliyompa ya ushauri wa ufundi.
“Yalikuwa ni makubaliano baina ya wanamichezo wawili, sioni kosa lolote katika jambo hilo,” alisisitiza Blatter ambaye ana umri wa miaka 85.
Platini mwanasoka wa zamani wa Ufaransa aliyewahi kutwaa taji la Ulaya akiwa nahodha wa timu ya Taifa ya Ufaransa mwaka 1984, alisaini mkataba kwa ajili ya kazi hiyo mwaka 1999 lakini mkataba wake inadaiwa ulitaja malipo ya Pauni 244,809 pekee bila malipo mengine ya nyongeza.
Platini anadaiwa kuwasiliana na Fifa mwaka 2011, akidai malipo hayo na ndipo walipomtaka awasilishe madai rasmi, jambo ambalo alilifanya na kulipwa baada ya siku 10 ingawa waendesha mashitaka nao wanadai kuwa Blatter aliidhinisha malipo ya jumla ya Pauni 1.6 milioni kwa Platini kinyume na taratibu.
Kuhusu kuchelewa kulipwa fedha hizo hadi mwaka 2011, Platini aliiambia mahakama kuwa alichelewa kuwasilisha madai ya malipo hayo kwa sababu hakuwa na uhitaji wa fedha hizo na alifanya hivyo aliposikia kuna waajiriwa wa Fifa walipewa fedha walizokuwa wakidai kwa muda mrefu.
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Uswisi inawatuhumu Blatter na Platini kwa ufisadi na matumizi mabaya ya fedha pamoja na kughushi nyaraka. Vigogo hao mwaka 2016 wote walifungiwa kujihusisha na soka.
Kwa upande mwingine Platini anadai kuwa tuhuma hizo ni mpango maalum uliotengenezwa ili kumzuia katika dhamira yake ya kugombea nafasi ya urais wa Fifa katika uchaguzi wa mwaka 2015 akipania kumrithi Blatter. “Nilichofanyiwa na Fifa ni kutengenezewa kashfa na lengo ni kuhakikisha siwi Rais wa Fifa,” alisema.
Kimataifa Blatter akana kumlipa Platini kifisadi
Blatter akana kumlipa Platini kifisadi
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
