Na mwandish wetu
Bodi ya Ligi Kuu Bara imetangaza rasmi kuwa bingwa wa michuano hiyo atazawadiwa Shilingi milioni 600 na kombe jipya lililozinduliwa.
Kiasi hicho kinatokana na zawadi ya bingwa ya Shilingi milioni 100 kilichotangazwa kutolewa na mdhamini wa ligi hiyo, Benki ya NBC huku milioni 500 nyingine ikiwa ni zawadi kutoka kwa Azam Media wenye haki ya matangazo ya mechi za ligi.
Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Almasi Kasongo alitangaza pia na zawadi za washindi wengine alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam huku akitaja kuwa timu zitakazoshuka daraja zitapewa mchango wa milioni 10 na bodi ya ligi kama maandalizi ya msimu ujao.
“Ligi Kuu ya NBC ina washiriki 16, kwa mujibu wa kanuni ina wajibu wa kutoa bingwa, mshindi wa pili na wa tatu. Tuna zawadi aina mbili, zawadi za ‘bonus’ kupitia mkataba tulioingia na Azam Media kuanzia kwa bingwa mpaka wa mwisho.
“Mchanganuo ni kama ifuatavyo bingwa atakuwa na zawadi mbili za fedha, zawadi ya kwanza ni bonus ya Azam Media ambayo ni Shilingi milioni 500 ambayo itaambatana na zawadi ya NBC Sh milioni 100, hivyo jumla atapata milioni 600,” alisema Kasongo.
“Mshindi wa pili atapata Sh milioni 250 za Azam na Sh milioni 50 kutoka NBC, wa tatu atapata Sh milioni 225 na Sh milioni 30 kutoka NBC,” alisema Kasongo.
Kasongo alisema zawadi nyingine kuanzia mshindi wa nne ni Sh milioni 200 mpaka Sh milioni 20 kwa timu itakayoshika nafasi ya 14 itakayocheza ‘play-off’ kuwania kusalia Ligi Kuu huku Bodi ya Ligi ikiwachangia Sh milioni 10 kwa timu mbili zitakazoshuka kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya ua mwa Championship.
Kuhusu kombe jipya la bingwa lenye muundo mpya litakaloanza kutumika msimu huu, Kasongo alisema kombe hilo limebuniwa kwa kuzingatia thamani kubwa ya ligi yenyewe ya NBC.
“Kwa takwimu za rekodi za CAF (Shirikisho la Soka Afrika) ligi yetu ni ya 12 kwa kupata fursa ya kutoa wawaikilishi wanne (michuano ya klabu ya Afrika) hivyo tuliwaomba watufanyia kazi hii ya kubuni kombe iendane sambamba na thamani ya ligi yetu tuliyonayo hivyo baada ya kujiridhisha, tumelipitisha na sasa tunalitangaza rasmi,” alisema Kasongo.
NBC ambao Oktoba, mwaka jana wameingia kandarasi ya miaka mitatu wa kuidhamini ligi hiyo kwa Sh bilioni 2.5 wamekuwa na nyongeza ya Sh milioni 20 kwa bingwa ikiwa ni tofauti na zawadi ya Sh milioni 80 iliyokuwa ikitolewa na Kampuni ya Vodacom iliyokuwa ikidhamini ligi hapo awali.
Yanga ndiyo timu inayopewa nafasi kubwa ya kulibeba taji hilo ikiwa inahitaji pointi tatu katika mechi nne zilizobaki ili kutangazwa bingwa.
Soka Bingwa Ligi Kuu kupewa milioni 600, kombe jipya
Bingwa Ligi Kuu kupewa milioni 600, kombe jipya
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
