Na mwandishi wetu
Mkurugenzi wa Mashindano Yanga, Thabiti Kandoro amesema kikosi cha timu hiyo kinaendelea na maandalizi makali ili kumaliza kwa ushindi mechi zilizosalia licha ya kuwa wanawania pointi tatu pekee kutawazwa mabingwa wapya wa Ligi Kuu ya NBC.
Kandoro ameeleza kuwa kikosi hicho kinaendelea na maandalizi yake Avic Town, Kigamboni kama kawaida kwa kuwa wanahitaji kumaliza ligi vizuri na kutunza rekodi waliyonayo ya kutopoteza mchezo mpaka sasa.
Yanga inaongoza ligi kwa pointi 64 dhidi ya Simba inayoshikilia nafasi ya pili kwa pointi 51. Yanga inahitaji pointi moja kwenye michezo minne iliyosalia ili kunyakua rasmi ubingwa huo.
“Tunaendelea na mazoezi kama kawaida chini ya program ya kocha Nabi (Nasreddine) kwa ajili ya mechi inayofuata ya Coastal Union, tumeendelea siku zote hizo tukipumzika kwa siku nne tu tangu ilipoanza kalenda ya mechi za Fifa.
“Tuna malengo makubwa ya kufanya vizuri katika mechi zilizobaki, tunapambana kupata ubingwa hivyo hata kama ni pointi moja hatuwezi kujiachia au kuona ni kitu rahisi kukipata, huko ni kuudharau mpira na mpinzani,” alisema Kandoro.
Mkurugenzi huyo pia alisema jambo jingine ni kuendelea kuwapa burudani na ushindi kila wakati mashabiki wake mpaka mwisho ili kuunyakua ubingwa huo kwa mechi za ushindi mpaka mwisho wa msimu.
Yanga ambayo haijatwaa ubingwa huo kwa misimu minne mfululizo, mpaka sasa haijapoteza mchezo wowote kwenye ligi ikiwa imeshinda mechi 19 na sare saba, pia imefunga mabao 42 ikiwa ni idadi kubwa zaidi na kuruhusu mabao saba ambayo ni machache zaidi kwenye ligi.
Yanga itaanza kwa kuivaa Coastal Union, Juni 15 mwaka huu kabla ya kukipiga na Mbeya Kwanza kisha Mbeya City na kufunga pazia rasmi dhidi ya Mtibwa Sugar.
Soka Yanga yapania kumaliza ligi kishujaa
Yanga yapania kumaliza ligi kishujaa
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
