Na Jonathan Haule
Tusisahau tulipotoka, tukumbushane zama ambazo timu ya soka ya Taifa ya Wanawake ya Twiga Stars inatoka Dar es Salaam hadi Zimbabwe kwa basi.
Wachezaji wakiwa kwenye gari aina ya Toyota Coaster mali ya TFF (FAT) wanasafiri zaidi ya kilometa 1,500 wakifika huko wamechoka wanaamkia kwenye mechi ngumu, wanafungwa mabao mengi na kurudi nyumbani.
Baada ya kipigo wachezaji na makocha wao wanarejea Dar es Salaam na gari ile ile, wanachoka na wengine kufikia hospitali kwa matibabu, baadaye unawakuta wachezaji hao hao ofisi za TFF wakisotea posho zao.
Ni zama ambazo usingeweza kuwaza kama kuna siku Tanzania ingeweza kufuzu fainali za Kombe la Dunia, huo ni wakati ambao kuna watu waliokuja na mawazo ya kuitaka TFF iachane na soka la wanawake.
Ilikuwa hoja sahihi ukiangalia mazingira ya timu yalivyokuwa zama hizo, timu ilikuwa ya kufungwa mabao mengi, ni zama ambazo hamasa ilikuwa chini, Twiga ilikua kama timu ya wilaya ya Kinondoni, eneo ambalo walau kulikuwa na hamasa kwenye soka la wanawake.
Ilionekana kama waliokuwa wakiongoza soka enzi hizo walikurupuka kwenye soka la wanawake wakati uwezo kifedha ulikuwa mdogo, mipango hakukuwa na mipango sahihi, bajeti ndogo au isiyokidhi mambo ya msingi au haikuwapo kabisa, ilikuwa kama timu inayoendeshwa kwa kutembeza bakuli.
Habari ya soka la wanawake Tanzania leo hii inahusisha timu iliyofuzu kushiriki fainali za Kombe la Dunia nchini India. Tuna kila sababu ya kuipongeza Serengeti Girls kwa kufuzu kushiriki fainali hizo za wasichana chini ya miaka 17.
Tuwapongeze wachezaji na wote walioshiriki kuiwezesha timu kufuzu, kuanzia wachezaji, viongozi wa TFF, makocha na wote waliohusika kwa namna moja au nyingine kuifikisha Serengeti Girls ilipofika.
Katika hali ya kawaida leo ilitakiwa iwe siku kubwa na ya kihistoria, timu hiyo inakuwa ya kwanza katika soka kufuzu fainali za Kombe la Dunia ukiacha ile ya walemavu, hivyo kimsingi ni timu inayoanzisha historia mpya ya soka nchini.
Shamrashamra zilitakiwa kuanzia jana na kumalizia leo kwa watu kufurahia mafanikio ya timu hiyo ambayo ni ya kihistoria.
Naamini hali ingekuwa tofauti kama Taifa Stars au Serengeti Boys ingekuwa ndiyo iliyofuzu Kombe la Dunia, timu ingepokewa kuanzia kituo cha basi, bandarini au uwanja wa ndege kwa shamrashamra za kila aina, hali isingekuwa ilivyo sasa, kelele na hali inayoashiria ushindi ingejidhirisha kila kona.
Hatuwezi kulinganisha soka la wanawake na lile la wanaume kwa Tanzania katika hamasa, soka la wanaume hamasa ipo juu, si Tanzania tu bali duniani kote kwani wakati mwingine hata wanawake wenyewe baadhi yao ni mashabiki wa soka la wanaume kuliko lile la wanawake.
Kinachoonekana kwa Serengeti Girls sababu mojawapo ni hiyo lakini ya pili ni kazi ya kuitangaza timu hiyo haijafanyika, wakati ikipata ushindi mnono, kwa mfano ushindi wa mabao 7-0 dhidi ya Botswana halikuwa jambo kubwa wakati vipigo vya aina hiyo ndivyo Twiga Stars ilikuwa ikikutana navyo.

Leo hii ni kama Serengeti imefanya mapinduzi ya ushindi kwenye soka la wanawake, imepindua meza ya mafanikio kutoka kufungwa mabao mengi na kuaga mashindano mapema hadi kufunga mabao mengi na kufuzu hatua ya fainali, hili nalo linahitaji pongezi.
Kwa maana nyingine Tanzania imetoka katika soka la wanawake la wasindikizaji hadi kuwa timu mshindani tishio, naamini inakwenda India Oktoba mwaka huu kwenye fainali za Kombe la Dunia ikiwa moja ya timu tishio kutoka Afrika.
Nchini India kwa Afrika, Serengeti itaungana na timu za Nigeria na Comoro lakini hapo hapo kuna timu za Brazil, Canada, Marekani, Japan, Mexico, China, Hispania, Colombia, Ujerumani, Ufaransa, Chile, New Zealand na India ambao ni wenyeji wa mashindano hayo.
Kushindwa kuipongeza kwa kiwango cha mafanikio yao ni jambo moja lakini kuna jambo la muhimu la maandalizi ya timu ambayo ni muhimu yakaanza sasa kwani kuna hatua kutoka sasa hadi Oktoba.
Ikiwezekana si vibaya timu hiii ikatafutiwa safari ya maandalizi nje ya nchi kwa lengo la kuiweka katika mazingira mazuri ya kiushindani pamoja na mambo mengine muhimu yanayohusu maandalizi ya timu ambayo kimsingi imeiheshimisha Tanzania.
Naamini hata kwenye fainali za Kombe la Dunia inaweza kufanya maajabu na kuzidi kuiheshimisha Tanzania kama itapewa maandalizi ya uhakika yenye hadhi ya fainali za Kombe la Dunia.
Nasema hivyo kwa sababu timu hii imenikumbusha tulipotoka, zama zile tukiamini haiwezekani lakini wao wamedhihirisha kwamba inawezekana, jambo la msingi ni maandalizi.
