Na mwandishi wetu
Naibu Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo, Pauline Gekul amewapongeza wote walioshiriki kufanikisha timu ya taifa ya wasichana chini ya miaka 17 kufuzu fainali za Kombe la Dunia.
Sambamba na hilo, waziri huyo pia alisisitiza umuhimu wa kuishika mkono vilivyo timu hiyo kwa kuwa wasichana hao wameliheshimisha taifa.
Kauli ya waziri huyo imekuja baada ya timu hiyo au Serengeti Girls jana kuibuka na ushindi wa bao 1- dhidi ya Cameroon kwenye Uwanja wa Amaan na hivyo kushinda kwa jumla wa mabao 5-1 baada ya ushindi wa awali wa mabao 4-1 na hivyo kukata tiketi ya kushiriki michuano hiyo inayotarajia kufanyika India kuanzia Oktoba 11 mpaka 30, mwaka huu.
Gekul alisema kuwa wameweza kufanya hivyo kutokana na upendo na ushirikiano mkubwa waliokuwa nao kama timu na kuonesha pia inawezekana kama Watanzania wakiamua kuzungumza lugha moja kama ambavyo wamekuwa wakisisitiziwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
“Kwa namna ya kipekee kwanza nimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, amekuwa akitusukuma kwamba Watanzania kila siku tunashindwa sasa tunahitaji kushinda, nishukuru sana kwa jinsi Rais Samia ambavyo ametuelekeza wizara yetu chini ya Waziri Mohammed Mchengerwa ambaye amenituma huku kuja kushiriki na timu yetu siku zote, ambacho naweza kusema Watanzania tunaweza, suala ni maamuzi tu kutenga muda lakini pia kuwa makini na jambo letu.
“Niwashukuru sana wenzetu ambao wametenga muda, makocha wetu, TFF, Mkurugenzi wetu wa michezo, Baraza la Michezo Tanzania na timu nzima ya Serengeti Girls ambao kiukweli wametuheshimisha, hili jambo si jepesi, vijana wetu wamevumilia sana hatuna cha kuwalipa.
“Kwa hiyo Watanzania wenye vipaji waendelee kujitokeza mambo ndiyo hayo Mungu ameweka mkono wake, kubwa zaidi ni upendo na ushirikiano katika kazi kama timu tumefanya kazi kwa upendo na ushirikiano kwa hiyo jitihada hizi ni kwa sababu tunaongea lugha moja na sisi tumemuelewa Rais kwa hiyo tuendelee kushikamana tutaendelea kufanya makubwa, hatuwezi kuwaacha watoto wametuheshimisha Mungu awalinde awape afya njema waendelee kuitangaza Tanzania,” alisema Gekul.
Timu hiyo imefanikiwa kufuzu michuano hiyo iliyoshindwa kufanyika mwaka jana kutokana na janga la corona baada ya kuibugiza Botswana mabao 11-0 baada ya ushindi wa mechi mbili za nyumbani na ugenini kisha kuifunga Burundi kwa ushindi wa jumla wa mabao 5-2 kabla ya kukutana na Cameroon.
Serengeti sasa wanaungana na timu za Nigeria na Morocco ambao ni wawakilishi wengine kutoka Afrika katika idadi ya timu 16 zinazokwenda kuwania ubingwa huo wa Dunia.
Timu nyingine ni wenyeji India, Mexico, Ufaransa, Colombia, Japan, Chile, Canada, China, Marekani, Brazil, New Zealand, Ujerumani na Hispania.
Soka Waziri Gekul aipa tano Serengeti Girls
Waziri Gekul aipa tano Serengeti Girls
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
