Algeria yashika usukani Kundi F
Algeria jana usiku iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Uganda Cranes katika mechi ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2023) na hivyo kushika usukani wa Kundi F.
Ushindi huo wa nyumbani unawafanya Algeria kufikisha pointi tatu na mabao mawili na hivyo kuongoza kundi hilo ambalo pia lina timu za Niger na Taifa Stars ambao nao walicheza jana na kutoka sare ya bao 1-1 katika mechi ya awali wakati Uganda inashika mkia.
Algeria ambao pia ni mabingwa wa Afcon 2019 waliandika bao lao la kwanza katika dakika ya 28 lililofungwa na Aissa Mandi ambaye aliuwahi mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na Youcef Belaili na kutemwa na kipa wa Uganda.
Juhudi za Uganda kusaka bao zilianza kuonyesha dalili za kuzaa matunda muda mchache kabla ya timu kwenda mapumziko baada ya kupata penalti ambayo hata hivyo mpigaji Faruk Miya alishindwa kuujaza mpira wavuni baada ya shuti lake kudakwa na kipa wa Algeria, Mustapha Zeghba. Penalti hiyo ilitolewa baada ya Rachid Ghezzal kumchezea rafu Isaac Muleme wa Uganda.
Zikiwa zimebaki dakika 10 mpira kumalizika, Belaili aliipatia Algeria bao la pili baada ya kuwahadaa wachezaji watatu wa Uganda kabla ya kuujaza mpira wavuni. Algeria sasa inasubiri kuumana na Taifa Stars katika mechi itakayopigwa Juni 8 mwaka huu.
Katika mechi nyingine za Afcon 2023 matokeo ni kama ifuatavyo…
Tunisia 4-0 Equatorial Guinea
Rwanda 1-1 Msumbiji
Libya 1-0 Botswana
Niger 1-1 Tanzania
Dr Congo 0-1 Gabon
Mauritania 3-0 Sudan
Burundi 1-1 Namibia
Gambia 1-0 Sudan Kusini
Burkina Faso 2-2 Cape Verde
Ivory Coast 3-1 Zambia
Comoro 2-0 Lesotho
Togo 2-2 Eswatini (Swaziland) Mali 4-0 Congo
Senegal 3-1 Benin
