Na mwandishi wetu
Vuguvugu linaloendelea Simba kwa sasa, hatimaye limemuibua mwenyekiti wa zamani wa timu hiyo, Swed Nkwabi na kueleza kuwa yanayoendelea sasa kwa timu hiyo ni mwanzo tu, mengi yataibuka.
Hivi karibuni, Simba imekuwa kwenye migogoro kwa baadhi ya wajumbe wa kamati ya utendaji kulalamika namna timu inavyoendeshwa na hata namna inavyopata matokeo mabovu kiasi cha kupelekea juzi kutimuliwa kwa kocha wa timu hiyo, Pablo Franco.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Nkwabi alisema kwa ujumla mambo hayakuwa mazuri tangu mwanzo wakati yeye akiwa kwenye timu hiyo ndiyo maana aliamua kukaa kando na kusubiri muda utoe matokeo yake.
“Mambo kwa ujumla hayakuwa mazuri tangu mwanzo, tulichokosea ni kwamba hatukufuata utaratibu wa mabadiliko ya uendeshaji, kwa ukubwa wa Simba kama vitu vimekamilika ilipaswa watu waelezwe vizuri lakini watu wanafanya vificho vificho kama ni kitu cha mtu mmoja au binafsi, haifai hiyo.
“Ni hivi, kama imefikia hatua wajumbe wa bodi wanakuja kuongea kwenye media hawaongei kwenye bodi ina maana kuna matatizo, sehemu ambayo mtu unatakiwa wewe ndiyo utoe maamuzi unashindwa, unakwenda kulalamika nje, ndiyo maana mimi nilitoka nikasema muda utaongea.
“Nahisi hapo bado, watu hawajaanza kuongea, naweza kusema kuna upuuzi unaendelea ndani ya Simba. Sababu utaratibu wa mabadiliko hautaki kufuatwa, utaratibu wa makubaliano kati ya mwekezaji na Simba hauendi sawasawa. Watu sasa lazima wakae chini, wakae mezani, wajue wapi kuna shida maisha yaendelee,” alisema Nkwabi ambaye aling’atuka Simba mwaka 2019.
Ikumbukwe kuwa hivi karibuni wajumbe wa bodi, Mwina Kaduguda na Kassim Dewji walihojiwa na vyombo vya habari wakifafanua kuwa kuna maamuzi mengi yamefanyika Simba na hayakuwa sahihi ikiwemo mambo ya usajili na kufukuzwa kwa Pablo.
Dewji alikwenda mbali na kumtaja Mtendaji Mkuu wa timu hiyo, Barbara Gonzalez kuwa anahusika kumbana katika utendaji wake akiwa kama mwenyekiti wa kamati ya usajili ya timu hiyo.
Kuhusiana na hilo, Nkwabi alisema: “Mimi sipo kwenye uongozi siwezi kujua utendaji wake ukoje, siwezi kumzungumzia mtu ambaye sijafanya naye kazi isipokuwa mimi nasikia tu kama watu wengine wanavyosikia kwamba utaratibu wake si mzuri, lakini mimi sijui chochote hata kigezo gani kilitumika kumpa kazi sijui kwa hiyo siwezi kuongea chochote.”
Mvurugano huo wa Simba umeibuka tangu timu hiyo ilipotolewa nusu fainali ya Kombe la FA na Yanga na kuzima ndoto za kuitetea ndoo hiyo, kama inavyoonekana kushindwa pia kuutetea ubingwa wake wa ligi usitue kwa Yanga baada ya kuutwaa misimu minne mfululizo iliyopita.
Kutolewa pia kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na Orlando Pirates ya Afrika Kusini kwenye hatua ya robo fainali kumetajwa kuchangia kuondolewa kwa kocha huyo raia wa Hispania.
Soka Nkwabi atema nyongo Simba
Nkwabi atema nyongo Simba
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
