Na mwandishi wetu
Sare ya bao 1-1 ya Yanga dhidi ya Biashara United haijalifurahisha benchi la ufundi la timu hiyo na wamekiri kuwa makosa ya safu ya ulinzi ya timu yao yamewaponza hadi kukosa pointi tatu.
Katika mchezo huo uliopigwa jana kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza Yanga ilihitaji pointi tatu ili kuusogelea zaidi ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu lakini sasa italazimika kuzitafuta pointi tatu kwenye mchezo wao unaofuata dhidi ya Coastal Union ili kutawazwa mabingwa wapya.
Kocha Msaidizi Cedric Kaze alisema walistahili kuimaliza mechi kipindi cha kwanza kutokana na nafasi takriban nne za kufunga walizozipata lakini baada ya kupata bao la kuongoza kipindi cha pili, walipoteza umakini na mabeki waliruhusu bao ambalo hawakustahili kufungwa kutokana na ukubwa wao.
“Tulipaswa kupata ushindi tangu kipindi ha kwanza, tulipata nafasi karibu tatu au nne za kufunga lakini hatukuzitumia na kwenye mechi hizi ukienda mpaka mapumziko sare unampa kujiamini zaidi mpinzani wako na mechi inakuwa ngumu.
“Tulipata bao la kwanza kipindi cha pili lakini kukakosekana umakini baada ya hapo maana haiwezekani ushafunga bao moja halafu unafungwa kwenye boksi lenu mpo wawili, ni makosa ya kitaaluma naona tunapaswa kukaa na kujitathimini, haya mambo yanakuwaga kwenye timu za watoto.
“Tunapaswa kujilinda zaidi, sana sana tukiwa tumefunga na tunaongoza lakini yote ya yote tumeipokea pointi moja na pia tumecheza na timu imetupa ushindani tunajipanga na mechi ijayo,” alisema.
Yanga ilifunga bao dakika ya 75 kupitia kwa Fiston Mayele, bao ambalo lilidumu kwa dakika tatu kabla ya Collins Opare kuchomoa bao hilo dakika ya 78.
Naye kocha mkuu wa Biashara United, Vivier Bahati alieleza namna walivyokuwa wakiufahamu uwezo wa Yanga na kucheza kwa nidhamu dhidi yao huku akifunguka pia namna alivyomdhibiti kiungo wa Yanga, Zawadi Mauya na kuziba mianya ya wao kushambuliwa zaidi.
“Tulikuwa tunajua uwezo wa Yanga, ukiwaruhusu wacheze wanafanya kitu kizuri, kwa hiyo tuliwaacha wacheze kwao, tukawa tunasubiri wakija kwetu tunakuwa wengi tunachukua mpira lakini kipindi cha pili ilibidi tuongeze mshambuliaji ili tuongeze pia nguvu yetu ya kushambulia.
“Tuliruhusu goli jepesi lakini tulipata nguvu dakika chache na kurudisha goli, inaonekana tulituliza vichwa vizuri. Unajua tulifanya mabadiliko ili kuingiza washambuliaji ambao wanaweza kuanza kukabia juu na kumzuia Mauya asipige pasi nyingi kuja kwetu na hilo pia tulifanikiwa,” alisema.
Yanga imesalia kileleni na pointi zake 64 baada ya mechi 26 dhidi ya mabingwa watetezi Simba inayoshikilia nafasi ya pili ikiwa na pointi 51 baada ya mechi 25.
Soka Yanga yajilaumu sare ya Biashara
Yanga yajilaumu sare ya Biashara
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
