London, England
Kiungo wa Man City, Kevin de Bruyne ametwaa tuzo ya mwanasoka bora wa msimu wa 2021/22 wa Ligi Kuu England ikiwa ni mara yake ya pili sasa kufanya hivyo huku mchezaji mwenzake, Phil Foden naye akitwaa tuzo ya mwanasoka bora mwenye umri mdogo.
Awali mshambuliaji wa Liverpool, Mohamed Salah ambaye ameifungia Liverpool jumla ya mabao 22 hadi sasa na ndiye kinara wa mabao katika Ligi Kuu England alikuwa akitajwa mno kuibeba tuzo hiyo msimu huu.
De Bruyne mwenye umri wa miaka 30, ameifungia City mabao 15 msimu huu wakati timu hiyo jioni ya leo ikimtegemea katika kuhakikisha inalitwaa taji la Ligi Kuu England ikiwa katika mbio hizo na Liverpool.
“Kushinda tuzo hii kwa mara ya pili ni mafanikio, najivunia hilo,” alisema akiizungumzia tuzo hiyo ambayo alikuwa akiwania na mchezaji mwenzake wa City, Joao Cancelo na Mohamed Salah na Trent Alexander-Arnold wa Liverpool.
Katika orodha hiyo pia walikuwamo Jarrod Bowen wa West Ham, Bukayo Saka wa Arsenal, Son Heung-min wa Tottenham na James Ward-Prowse wa Southampton. Mara ya kwanza kwa De Bruyne kutwaa tuzo hiyo ilikuwa ni msimu wa 2019/20 na hivyo anaungana na wanasoka wengine kina Cristiano Ronaldo, Thierry Henry na Nemanja Vidic ambao wameibeba tuzo hiyo zaidi ya mara moja.
Baada ya kutwaa tuzo hiyo, De Bruyne alielezea kufurahishwa kwake kwa namna ambavyo msimu wa Ligi Kuu England umekuwa mzuri kwa upande wake kwa msimu huu kama ilivyo kwa katika tuzo hiyo ambao alisema nao wamekuwa na msimu mzuri katika klabu zao.
Kinachosubiriwa sasa ni kuona nini atakifanya mchezaji huyo kutoka Ubelgiji pamoja na Foden ambaye pia ni mchezaji wa England katika kuhakikisha City inalibeba taji la England msimu huu.
Kimataifa De Bruyne atwaa tuzo mbele ya Salah
De Bruyne atwaa tuzo mbele ya Salah
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
