Paris, Ufaransa
Baada ya wiki ya maswali yasiyo na majibu hatimaye kiungo Kylin Mbappe ameamua kubaki katika klabu ya PSG ya Ufaransa na kuachana na Real Madrid ya Hispania.
Uamuzi huo licha ya kumaliza kitendawili cha hatima ya mchezaji huyo umeacha balaa baada ya mabosi wa Ligi Kuu Hispania (La Liga) kutangaza nia yao ya kuishitaki PSG kwa kukiuka kanuni za biashara na kufanya ushawishi usiofaa katika usajili huo.
Mbappe ambaye mkataba wake na PSG ulikuwa ufikie mwisho Juni 30 mwaka huu tayari amesaini mkataba mwingine unaodaiwa kuwa wa miaka mitatu na klabu hiyo hatua ambayo imewashitua watu wengi waliokuwa wakimfuatilia hasa baada ya kuhusishwa na mipango ya kuhamia Real Madrid, mipango ambayo hadi majuzi ilidaiwa kufikia hatua nzuri.
Usajili huo ulikuwa mjadala licha ya Mbappe mwenyewe kutokuwa wazi, aliishia kusema kwamba kila kitu kingejulikana hivi karibuni na kwamba aliamua kukaa kimya ili kuheshimu pande mbili zilizokuwa zikimjadili yaani PSG waliotaka kumbakisha na Real Madrid waliotaka kumng’oa Ufaransa.
Nchini Hispania habari zinadai kuwa mabosi wa La Liga wamekerwa na uamuzi huo wa Mbappe na katika azma yao ya kulifikisha suala hilo kwenye vyombo vya sheria watashitaki katika mamlaka za soka Ufaransa, Uefa pamoja na Umoja wa Ulaya.
Inadaiwa kwamba Mbappe alishakubaliana na Madrid kuhusu maslahi yake binafsi na kilichokuwa kikisubiriwa ni mambo madogo ya mwisho kabla ya kujiunga na klabu hiyo kabla ya kubadili mawazo na kuamua kubaki Ufaransa jambo ambalo sasa inadhaniwa kwamba kuna mchezo usio mzuri kibiashara ambao umefanywa na PSG.
Habari zaidi zinadai kwamba PSG imetumia fedha nyingi mno kumbakisha Mbappe na kumfanya awe mchezaji anayelipwa fedha nyingi duniani kuanzia mshahara wake wa wiki ambao inadaiwa utafikia Pauni 1 milioni jambo ambalo nchini Hispania linaonekana kuwa ni kutumia fedha kufanya ushawishi mbaya pamoja na matumizi mabovu ya fedha yanayoharibu hadhi na heshima ya soka.
Mbappe mwenye umri wa miaka 23 akizungumzia uamuzi wake wa kuongeza mkataba na PSG alisema kwamba anafurahia uamuzi huo ambao umetokana na mazungumzo yaliyofanywa na wakala wa mchezaji huyo na rais wa klabu ya PSG, Nasser Al-Khelaifi.
“Naamini nikiwa hapa nitaendelea kukuza kiwango changu katika klabu hii ambayo imejiwekea kila kitu cha kuifanya ifanikiwe na kuwa katika kiwango cha juu, pia nafurahia kuendelea kucheza sokaUfaransa, nchi ambayo nimezaliwa na kukulia,” alisema Mbappe.
Kimataifa Mbappe abaki PSG, azua balaa
Mbappe abaki PSG, azua balaa
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
