London, England
Kiungo wa Chelsea, Mateo Kovacic huenda akaikosa mechi ya fainali ya Kombe la FA dhidi ya Liverpool keshokutwa Jumamosi baada ya kuumia enka.
Kocha wa Chelsea, Thomas Tuchel ameelezea wasiwasi wa kumkosa mchezaji huyo ambaye aliumia wakati akikabiliana na Daniel James wa Leeds katika mechi ya Ligi Kuu England ambayo Chelsea iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 na James kupewa kadi nyekundu baada ya tukio hilo.
Kovacic, staa wa zamani wa Real Madrid, licha ya kujitahidi kucheza lakini muda mfupi baadaye alilazimika kutoka nje ya uwanja akiwa katika maumivu.
Kwa sasa majaliwa ya mchezaji huyo kuiwakilisha Chelsea yako njia panda na haijaweza kufahamika mara moja iwapo atavaa jezi ya timu hiyo katika mechi hiyo muhimu ya kusaka taji la FA hasa baada ya Tuchel mwenyewe kuonyesha wasiwasi kuhusu mchezaji huyo kuwa fiti siku ya mechi.
“Lakini nawaambia mimi kama kocha si mtaalamu, uwezekano wa kucheza ni wenye kutilia mashaka, aliumia enka na alikuwa mwenye maumivu makali, ingawa mimi si daktari hivyo tunatakiwa kusubiri vipimo lakini matarajio ya kucheza hayapo, ni habari mbaya kwetu,” amesema Tuchel.
Tuchel ambaye katika mechi na Leeds alilazimika kuwapumzisha baadhi ya wachezaji muhimu akiwamo Kai Havertz na Thiago Silva ikiwa ni mkakati wa kusubiri kuivaa Liverpool sasa atalazimika kufikiria mara mbili kuhusu timu itakayoumana na Liverpool iwapo Kovacic hatakuwa fiti kwa wakati.
“Ni mtu muhimu kwenye safu yetu ya kiungo, alicheza dhidi ya Liverpool, nafikiri kwa mechi zote alicheza kuanzia mwanzo na alikuwa imara, ana njaa ya ushindi na mwenye kuvutiwa na mechi kubwa.” amesema Tuchel.
Soka Kovacic njia panda kuivaa Liverpool
Kovacic njia panda kuivaa Liverpool
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
