London, Uingereza
Baada ya Man City kushindwa katika hatua ya nusu fainali ya Ligi ya
Mabingwa Ulaya, uliibuka mjadala kuhusu hatima ya Kocha Pep Guardiol
katika klabu hiyo.
Mjadala huo umetokana na ukweli kwamba tangu atoke Barcelona, Pep
amekuwa akilifukuzia taji hilo bila mafanikio na msimu huu alionyesha
dalili za kufanikisha hilo lakini hatimaye mbio zake ziliishia nusu
fainali baada ya kutolewa na Real Madrid kwa jumla ya mabao 6-5.
Habari za ndani zinadai kuwa kocha yuko mbioni kusaini mkataba mpya
ambao utamuweka katika klabu hiyo hadi mwaka 2025 baada ya yeye
mwenyewe kuwahakikishia mabosi wake kwamba bado ana shauku kubwa ya
kulibeba taji hilo.

Hali pia iko hivyo hivyo kwa staa wa PSG ya Ufaransa, Kylian Mbappe
ambaye pia amekuwa akihusishwa na mipango ya kuondoka katika klabu
hiyo lakini habari za ndani zinadai kuwa Mfaransa huyo ataendelea
kukipiga PSG kwa mkataba mpya wa miaka miwili ambao thamani yake
inadaiwa kufikia Pauni zaidi ya milioni 40.
Hata hivyo habari nyingine zinadai kuwa mama mzazi wa mchezaji huyo,
Fayza Lamary amesema hana habari kuhusu mtoto wake kuwa mbioni kusaini
mkataba mpya PSG.
Kama ilivyo kwa Pep, Mbappe naye timu yake imekwama katika mbio za
kulisaka taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu na kuziachia vita
hiyo klabu za Liverpool na Real Madrid zitakazochuana Mei 28 mwaka huu
jijini Paris, Ufaransa.
