London, England
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta amewatetea wachezaji wake baada ya kipigo cha bao 1-0 mbele ya Everton juzi Jumamosi akisema kwamba sasa anawapenda zaidi.
Arsenal juzi ilipata kipigo cha pili katika Ligi Kuu England (EPL), kipigo hicho cha ugenini kimeshangaza wengi kwa kuwa Everton ni timu inayopambana kujinasua na janga la kushuka daraja wakati Arsenal ipo kileleni.
Bao hilo pekee la Everton lilipatikana dakika ya 60 mfungaji akiwa ni James Taarkowski aliyeunganisha kwa kichwa mpira uliopigwa na Dwight McNeil na kuwa ushindi wa kwanza katika mechi ya kwanza ya kocha mpya wa timu hiyo, Sean Dyche.
Wakati ushindi huo ukiibua matumaini ya Everton kujiondoa kwenye janga la kushuka daraja, kwa Arsenal ni pigo la pili katika EPL, mara ya mwisho ilifungwa na Man Utd Septemba mwaka jana.
Kipigo hicho hata pia hakijaitoa Arsenal kwenye mbio za kulisaka taji la EPL kwani Man City wanaoshika nafasi ya pili nao walilala kwa bao 1-0 mbele ya Spurs jana Jumapili.
Kwa hali hiyo Arsenal inaendelea kushika usukani wa EPL kwa tofauti ya pointi tano huku ikiwa na mechi moja pungufu, imecheza mechi 20 wakati City imecheza mechi 21.
“Kwa timu yangu nataka wafahamu kwamba nawapenda na nawapenda zaidi sasa kuliko ilivyokuwa saa tatu kabla, wiki moja kabla, mwezi, miezi mitatu kabla,” alisema Arteta.
“Ni jambo rahisi kuwa karibu na wachezaji wanaposhinda na kucheza vizuri, huu ni wakati ambao nawapenda wachezaji wangu zaidi, na kwa sasa tuko tumeshikamana pamoja,” alisema Arteta.
“Safari itakuwa ngumu, yenye changamoto na kutakuwa na mawe makubwa katikati ambayo tunatakiwa kuyakabili na sasa tunatakiwa kujiandaa vizuri hasa kwa ajili ya Jumamosi tuwe vizuri na tuliohamasika ili kuifunga Brentford,” alisema Arteta.
“Nafikiri Everton walikuwa vizuri hasa na kabla ya yote tunatakiwa kuwapongeza kwa namna walivyobadili mchezo na nafikiri walishinda kwa sababu walikuwa vizuri,” alisema Arteta.
Matokeo ya mechi za EPL wikiendi ni kama ifuavyo…
Nottingham Forest 1-0 Leeds United
Tottenham 1-0 Man City
Everton 1-0 Arsenal
Aston Villa 2-4 Leicester City
Brentford 3-0 Southampton
Brighton 1-0 Bournemouth
Man United 2-1 Crystal Palace
Wolverhampton 3-0 Liverpool
Newcastle 1-1 West Ham
Chelsea 0-0 Fulham
