Na mwandishi wetu
Kocha Msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze amewataka wachezaji wake kuzipa uzito mkubwa mechi za Kombe la FA kwani ndizo zinazotoa nafasi ya kushiriki mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Yanga ndio mabingwa watetezi wa taji hilo na kocha huyo ameeleza kuwa mikakati yao ni kuhakikisha wanalitetea tena ili kuwa na nafasi kubwa ya kushiriki mashindano ya kimataifa mwakani licha ya mpaka sasa pia kupigiwa chapuo ya kutwaa tena taji la Ligi Kuu NBC.
Kaze alisema baadhi ya wachezaji wao wamekuwa wakizidharau timu wanazokutana nazo kweye hatua hizi za awali kitu ambacho ni hatari sababu kwenye mpira chochote kinaweza kutokea bila kujali ukubwa wa timu.
“Wachezaji wetu hawapaswi kudharau wapinzani bila kujali ukubwa wao sababu huwezi kufika fainali kama hujazifunga timu ndogo ambazo umepangwa nazo huku chini maana katika mchezo wa soka lolote linaweza kutokea,” alisema Kaze.
Kocha huyo ameeleza kuwa mipango yao msimu huu ni kuendeleza kile walichokifanya msimu uliopita kwa kutwaa mataji yote ya ndani kitu ambacho anaamini wanakiweza kutokana na ubora wa kikosi walichokuwa nacho.
Alisema anajua vita ya kurudia kile walichokifanya msimu uliopita siyo ndogo lakini watapambana kuhakikisha walichokikusudia kinatimia kikamilifu ili kuendelea kuwafurahisha mashabiki wao.
Kwenye Ligi Kuu Yanga, ipo kileleni mwa msimamo ikikusanya pointi 56 na kwenye Kombe la FA wamepangwa kucheza keshokutwa Jumapili na Rhino Rangers ya Tabora.
