Na mwandishi wetu
Mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele na Kocha Mkuu wa Simba, Juma Mgunda wamechaguliwa kuwa Mchezaji Bora na Kocha Bora wa mwezi Novemba wa Ligi Kuu NBC.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Alhamisi na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imefafanua kuwa Mayele alionesha kiwango kizuri zaidi kwa mwezi huo na kuwapiku Saido Ntibazonkiza wa Geita Gold na Moses Phiri wa Simba.
Mbali na upinzani waliokuwa nao kwenye kinyang’anyiro hicho, Mayele na Phiri raia wa Zambia wamefungana kileleni pia kwenye idadi ya mabao msimu huu, kila mmoja akiwa amefunga mara 10 mpaka sasa.
Hata hivyo, katika mwezi huo, Mayele raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo alitoa mchango mkubwa kwa Yanga ikiwemo kufunga mabao saba huku akitoa pasi moja ya bao kwenye mechi tano alizocheza.
Mayele alifunga mabao matatu na kutoa ‘asisti’ kwenye ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Singida Big Stars kisha akafunga mabao manne katika michezo miwili ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Dodoma Jiji na Mbeya City.

Kwa upande wa Mgunda aliwashinda Hans Pluijm wa Singida BS na Mecky Maxime wa Kagera Sugar alioingia nao fainali, ambapo kwa mwezi huo Simba iliifunga Ihefu bao 1-0, ikailaza Ruvu Shooting mabao 4-0, ikaibamiza Polisi Tanzania mabao 3-1 kabla ya kutoka sare ya bao 1-1 na timu za Singida BS na Mbeya City.
Aidha, Kamati ya Tuzo za TFF katika kikao chake upande wa mchakato wa Kocha Bora kwa mwezi huo, haikuihusisha timu ya Azam kutokana na kutokuwa na kocha mkuu katika mwezi huo ingawa timu hiyo iliibuka na ushindi wa mechi zake zote tano za mwezi Novemba.
Pia, kamati hiyo imemchagua Meneja wa Uwanja wa Liti, Singida, Hassan Simba kuwa Meneja Bora wa Uwanja wa mwezi Novemba, kutokana na kufanya vizuri katika menejimenti ya matukio ya michezo pamoja na masuala yanayohusu miundombinu uwanjani.
