Doha, Qatar
Kocha wa Brazil, Tite amethibitisha kwamba mshambuliaji wake, Neymar leo Jumatatu jioni anatarajia kuwa uwanjani kuiwakilisha Brazil wakati ikiumana na Korea Kusini katika mechi ya kuwania tiketi ta robo fainali ya Kombe la Dunia.
Neymar alikosa mechi mbili za hatua ya makundi za timu hiyo baada ya kuumia enka ya mguu wa kulia katika mechi ya kwanza ya timu hiyo dhidi ya Serbia, mechi ambayo Brazil ilishinda kwa mabao 2-0 ingawa Neymar alitoka uwanjani dakika ya 80 huku akichechemea.
Brazil ni moja ya timu zinazopewa nafasi kubwa ya kubeba taji hilo, ikiwa Kundi G ilifuzu mapema hatua ya makundi baada ya kushinda mechi mbili licha ya kupoteza mechi yake ya mwisho ya hatua hiyo dhidi ya Cameroon ilipolala kwa bao 1-0.
Alipoulizwa jana Jumapili kuhusu Neymar kama atakuwa fiti na kucheza mechi dhidi ya Korea, Tite alisema, “ndio, Neymar atafanya mazoezi mchana na mazoezi yakienda vizuri atacheza.
Neymar ambaye pia anaichezea klabu ya Paris St-Germain ya Ufaransa aliumia baada ya kuchezewa rafu na Nikola Milenkovic wa Serbia na baadaye akasema kwamba majeraha aliyoyapata ni tukio zito katika maisha yake ya soka.
Mbali na Neymar, beki wa Brazil, Danilo naye inadaiw yuko fiti wakati Alex Telles na mshambuliaji Gabriel Jesus wameshaondolewa katika timu hiyo kwa ajili ya mechi za fainali za Kombe la Dunia kutokana na ukubwa wa majeraha yao.
Mechi za Kombe la Dunia leo Jumatatu…
Japan v Croatia
Brazil v Korea Kusini
