Doha, Qatar
Messi jana Jumamosi aliweka rekodi ya kufunga bao katika mechi yake ya 1,000 ya soka la hadhi ya juu na mechi ya 100 tangu awe nahodha wa timu ya Argentina iliyoilaza Australia mabao 2-1 na kufuzu hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia.
Akiwa katika fainali zake za tano za Kombe la Dunia kwa ushindi huo, Messi anazidi kufufua matumaini ya Argentina, moja ya timu inayopewa nafasi ya kulibeba taji hilo ambalo kwa mara ya mwisho ililibeba miaka takriban 36 iliyopita.
Bao la jana linakuwa la tisa kwa Messi kwenye fainali za Kombe la Dunia, anakuwa amevunja rekodi ya muda mrefu ya gwiji Diego Maradona mwenye mabao manane katika fainali hizo kama nyota mwingine wa zamani wa Argentina, Guillermo Stabile ingawa Messi bado ana kazi ya kuifikia rekodi ya nyota mwingine wa zamani wa timu hiyo, Gabriel Batistuta mwenye mabao 10.
Kwa Messi bao alilofunga dhidi ya Australia pia linakuwa bao la 789 katika maisha yake ya soka na akizungumzia mafanikio hayo, Messi alisema, ”nina furaha kwa kupiga hatua nyingine, kufanikisha malengo mengine, ilikuwa mechi ngumu.”
Mara baada ya mechi hiyo kumalizika, Messi alikuwa gumzo miongoni mwa mashabiki wa Argentina ambao mara kwa mara walikuwa wakiimba kwa kulitaja jina la mchezaji huyo.
“Ni tukio la kipekee, hakika nina furaha kujumuika na mashabiki katika tukio muhimu, najua juhudi walizochukua hadi kuja hapa na najua watu wa Argentina wote walipenda kuwa hapa, mshikamano na umoja tuliona ni jambo zuri,” alisema Messi mwenye miaka 35 sasa.
“Ni jambo ambalo huwezi kuamini, nguvu na furaha ni jambo la kipekee, mashabiki najua namna wanavyoumia na kufurahia, hilo ni jambo la aina yake, wana furaha kama ilivyo kwa watu wengine wote wa Argentina,” alisema.
Argentina sasa inasubiri kuvaana na Uholanzi katika mechi nyingine ambayo inatarajiwa kuwa ngumu na inayosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka duniani. Uholanzi inayonolewa na Luis Van Gaal ilifuzu robo fainali kwa kuichapa Marekani mabao 3-1.
Kimataifa Messi ni rekodi juu ya rekodi
Messi ni rekodi juu ya rekodi
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
