Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Tanzania Prisons, Patrick Odhiambo, ameeleza kukerwa na matokeo ya kupoteza michezo mitatu mfululizo na sasa anarejea kujipanga kuangalia amejikwaa wapi na kuyafanyia kazi madhaifu ya kikosi chake ili yasijirudie katika mchezo ujao na KMC.
Katika michezo mitatu iliyopita, Prisons imepoteza dhidi ya Kagera Sugar bao 1-0, Geita Gold mabao 4-2 na Coastal Union kwa mabao 2-0, matokeo yaliyowafanya washuke hadi nafasi ya 11 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC wakiwa na pointi 14.
Odhiambo alisema kuwa kama mwalimu hafurahishwi kabisa na kipindi anachopitia sasa baada ya kushindwa kupata pointi kwenye michezo mitatu iliyopita, hivyo atapambana kwenye uwanja wa mazoezi ili afute makosa yanayowanyima pointi.
“Hakuna mwalimu anayefurahi kuona anashindwa kupata matokeo katika michezo mfululizo hivyo nimeyaona mapungufu ya kikosi changu naenda kuyafanyia kazi makosa yote yaliyojitokeza katika michezo iliyopita ili tuweze kurudi kwenye staili tuliyoanza nayo msimu huu,” alisema.
“Huu ni mchezo muhimu kwetu (dhidi ya KMC) tunahitaji pointi tatu ili kurejesha hali ya kujiamini kikosini mwetu maana matokeo yaliyopita yanatuumiza na kuongeza wigo wa pointi dhidi ya walio juu yetu,” alisema Odhiambo.
Alisema kuwa huu ni wakati wa kushikamana na kuangalia madhaifu yao kitaalamu zaidi kabla ya kushuka uwanjani tena kuzisaka pointi tatu zitakazorudisha morali yao kikosini.
Prisons inatarajia kuumana na KMC Jumatatu ya keshokutwa kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.
Soka Prisons yajiuliza wapi ilipojikwaa
Prisons yajiuliza wapi ilipojikwaa
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
