
Doha, Qatar
Sasa ni rasmi, mshambuliaji, Sadio Mane hatokuwa na timu ya Senegal kwenye fainali za Kombe la Dunia baada ya kubainika kuwa maumivu aliyoyapata wiki iliyopita wakati akiichezea Bayern Munich katika mechi ya Bundesliga hayawezi kupona mapema.
Juzi Jumanne, Shirikisho la Soka Senegal lilitangaza kuwa mshambuliaji huyo tegemeo angekosa mechi ya kwanza ya michuano hiyo lakini baadaye vipimo zaidi vilifanyika na sasa imethibitishwa kwamba mchezaji huyo hawezi kabisa kucheza kwenye fainali Kombe la Dunia zitakazoanza Jumapili hii.
Baada ya kuumia wakati akiichezea Bayern dhidi ya Werder Bremen katika mechi ya Bundesliga, Mane mwenye umri wa miaka 30, alitoka nje katika dakika ya 20 na kuelezwa kwamba angeikosa mechi ya kwanza ya timu hiyo dhidi ya Uholanzi ambayo itachezwa Jumatatu ingawa taarifa za Bayern zilidai kuwa huenda akawa nje kwa siku 10.
Mane ambaye ana tuzo mbili za mchezaji bora wa mwaka wa Afrika, pia ndiye mfungaji wa bao la penalti lililowapa Senegal taji la Afrika katika mechi ya fainali dhidi ya Misri, Februari mwaka huu, kukosekana kwake katika timu ya Senegal linakuwa pigo kubwa kwani alitegemewa kuisaidia timu hiyo kufika mbali kwenye fainali za Kombe la Dunia.
