Na mwandishi wetu
Kocha wa timu ya soka ya wanawake ya Simba Queens, Charles Lukula amewapongeza wachezaji wake kwa jinsi walivyopambana na kumtupia lawama mwamuzi kwa alichodai kuwa alikuwa na maamuzi ya upande mmoja.
Simba Queens jana Jumatano ilitolewa katika mchezo wa nusu fainali wa Ligi ya Mabingwa Afrika na mabingwa watetezi, Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini baada ya kufungwa bao 1-0.
Katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Prince Heritier El Hassan mjini Rabat, Morocco, bao hilo pekee lilitosha kuzima ndoto za timu hiyo kucheza fainali ya michuano hiyo kwa mara ya kwanza.
Lukula alisema wachezaji wake walicheza vizuri lakini maamuzi ya mwamuzi yalikuwa ya upande mmoja kwani kuna mara kadhaa wachezaji wake walifanyiwa faulo lakini akaacha.
“Tulicheza vizuri kuanzia kipindi cha kwanza lakini bahati haikuwa yetu na mwamuzi kila faulo tuliyofanya alikuwa anatoa kadi ya njano lakini kwa upande wa wapinzani alikuwa anasema usirudie, ila nawapongeza wachezaji walicheza vizuri,” alisema Lukula.
Akimzungumzia nahodha wa kikosi hicho, mshambuliaji Opa Clement alisema mchezaji huyo anahitaji mtu wa kusaidiana naye ili akikosa kufunga mwingine afunge kuliko kumtegemea mmoja na kuongeza kuwa anatazamia mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu akitarajia watarudi na medali ya shaba.
Kwa matokeo hayo Mamelodi itacheza fainali Novemba 13 dhidi ya wenyeji AS FAR ya Morocco walioiingia fainali kwa kuifunga Bayelsa Queens ya Nigeria bao 1-0. Queens itacheza keshokutwa dhidi ya Bayelsa kutafuta mshindi wa tatu.
Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), bingwa wa michuano hiyo ataondoka na Dola za Marekani 400,000, mshindi wa pili Dola 250,000 na timu zilizocheza nusu fainali zitapata Dola 200,000 kila mmoja. Mshindi wa tatu atapata Dola 150,000, wakati itakayoshika nafasi ya nne itapata Dola 100,000.
Kimataifa Kocha Simba Queens amlaumu mwamuzi
Kocha Simba Queens amlaumu mwamuzi
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
