Munich, Ujerumani
Mshambuliaji nyota wa Senegal, Sadio Mane huenda akashindwa kwenda Qatar kuiwakilisha Senegal kwenye fainali za Kombe la Dunia baada ya kuumia jana Jumanne wakati akiiwakilisha Bayern Munich katika mechi dhidi ya Werder Bremen, mechi ambayo Bayern ilishinda kwa mabao 6-1.
Mane aliumia kwenye goti la kulia kwa chini na kulazimika kutoka nje ya uwanja baada ya dakika 20 za mchezo huo na nafasi yake kuchuliwa na Leroy Sane na sasa hofu iliyopo ni je mchezaji huyo ataweza kupona na hatimaye kuiwakilisha Senegal kwenye fainali za Kombe la Dunia ikiwa siku takriban 11 zimebaki kabla ya kuanza kwa fainali hizo.
Mchezaji huyo aliumia wakati akikimbia na kugombania mpira na mchezaji mmoja wa Bremen kabla ya kukaa chini na kuzungukwa na timu ya madaktari wa Bayern ingawa baadaye aliinuka taratibu na kujikongoja hadi kwenye vyumba vya kubadilishia nguo bila ya kubebwa.
Akizungumzia tukio hilo, kocha wa Bayern, Julian Nagelsmann alisema baada ya mechi hiyo kwamba mchezaji huyo atafanyiwa vipimo vya X-ray ili kujua ukubwa wa tatizo. “Kwa sasa siwezi kusema chochote kwa uhakika aliumia, ni tatizo la kwenye misuli, ni jambo lisilofurahisha,” alisema Nagelsmann.
“Nafikiri ni lazima afanyiwe vipimo vya X-ray ili kujua kuna tatizo gani lakini naamini hali si mbaya sana ingawa kimsingi kwa wakati huu siwezi kusema lolote kwa uhakika,” aliongeza Nagelsmann.
Mane amekuwa mchezaji muhimu wa Senegal, na ndiye aliyefunga bao la penalti ya ushindi dhidi ya Misri na kuiwezesha Senegal kubeba taji la Mataifa ya Afrika mapema mwaka huu na kumkosa kwenye fainali za Kombe la Dunia zinazoanza Novemba 20 mwaka huu itakuwa pigo kubwa kwa Senegal.
Senegal itatupa karata yake ya kwanza kwenye fainali za Kombe la Dunia Novemba 21 dhidi ya Uholanzi ikifuatiwa na mechi nyingine dhidi ya wenyeji Qatar na kumalizia mechi zake za makundi dhidi ya Ecuador.
Kimataifa Mane hatihati Kombe la Dunia
Mane hatihati Kombe la Dunia
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
