Madrid, Hispania
Atletico Madrid imeaga rasmi michuano ya klabu Ulaya, imetolewa Ligi ya Mabingwa na imekosa nafasi Europa Ligi baada ya kushika mkia katika kundi lake ikiwa ni mara ya kwanza kwa takriban miaka 10 ya kocha Diego Simeone wakati Tottenham imefuzu kibabe ikiwa kinara Kundi D.
Majanga ya Atletico yametokana na kipigo cha mabao 2-1 ilichokipata dhidi ya FC Porto katika mechi ya mwisho ya Kundi B jana Jumanne usiku wakati Spurs iliibuka na ushindi kama huo katika mechi ya mwisho ya kundi lake dhidi ya Marseille.
Matokeo mabaya ya Atletico yanakuwa majanga mengine kwa kocha Diego Simeone, kocha ambaye amekuwa na timu hiyo tangu mwaka 2011 na sasa ni mara ya kwanza kwa timu hiyo kutolewa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa ikiwa chini yake na kuaga kabisa michuano ya Ulaya mapema.
Mara mbili ambazo Atletico imetolewa hatua ya makundi kwenye Ligi ya Mabingwa yaani msimu wa 2009/10 na 2017/18 iliangukia Europa Ligi na ikabeba taji la michuano hiyo.
Kwa hali ilivyo sasa ni wazi kwamba Simeone atakuwa katika wakati mgumu kwani katika mechi 12 zilizopita za michuano mbalimbali, timu hiyo imeshinda mechi nne tu na hapana shaka kutolewa Ligi ya Mabingwa yanakuwa majanga juu ya majanga kwa Simeone.
Katika Kundi B, timu zilizofuzu ni Porto inayoshika usukani na Club Bruges wakati Bayer Leverkusen imeangukia Europa Ligi na Atletico imefika mwisho kwenye michuano ya Ulaya msimu huu.
Kocha mwingine aliyekuwa katika wakati mgumu ni Antonio Conte wa Spurs ambaye ushindi wa jana umepatikana wakati yeye akitumikia adhabu na hivyo hakuwa uwanjani, kabla ya mechi hiyo mazingira ya Kundi D pia yaliifanya Spurs kuwa njia panda isijue hatma yake kama inafuzu, inaangukia Europa au inaaga kabisa michuano ya Ulaya, mambo yote hayo yangewezekana.
Wakati Tottenham ikifuzu katika kundi hilo ikiwa kinara na pointi 11 pamoja na Frankfurt iliyoshika nafasi ya pili ikiwa na pointi 10, Sporting Lisbon inaangukia Europa Ligi ikiwa na pointi saba wakati Marseille iliyoshika mkia na pointi zake sita inaaga rasmi michuano hiyo.
Ushindi wa Spurs dhidi ya Marseille ni habari kubwa kwa mashabiki wa soka kwa namna ulivyopatikana baada ya timu hizo kupata sare ya bao 1-1 kabla Pierre-Emile Hojbjerg hajaifungia Spurs bao katika dakika tano za nyongeza na kuipa timu hiyo ushindi muhimu ambao si tu habari kubwa bali pia ni faraja kubwa kwa kocha Conte aliyekuwa akitumikia adhabu.
Matokeo mechi za jana Jumanne
Liverpool 2-0 Napoli
Rangers 1- 3 Ajax
B. Leverkusen 0-0 Club Bruges
FC Porto 2-1 Atlético Madrid
Bayern Munich 2-0 Inter Milan
Viktoria Plzen 2-4 Barcelona
Marseille 1-2 Tottenham
S. Lisbon 1-2 E. Frankfurt
Kimataifa Mambo magumu kwa Simeone Ulaya
Mambo magumu kwa Simeone Ulaya
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
