Manchester, England
Cristiano Ronaldo amerudi na baraka kikosini Man United baada ya kufunga bao katika ushindi wa 3-0 ambao timu hiyo iliupata jana Alhamisi katika mechi ya Europa Ligi dhidi ya Sheriff Tiraspol.
Ronaldo aliondolewa katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo na kukosekana katika mechi ya Jumamosi iliyopita dhidi ya Chelsea baada ya kukataa kuingia uwanjani akitokea benchi katika mechi na Tottenham Jumatano iliyopita na baadaye kususa na kutoka uwanjani kabla mechi hiyo kumalizika.
Mchezaji huyo hata hivyo alitoa kauli iliyoonyesha kujutia tukio hilo na kocha wake, Erik ten Hag akamruhusu kujiunga kwa mara nyingine na kikosi cha timu hiyo na jana akacheza mechi yake ya kwanza akianzia kipindi cha kwanza na kufunga bao hilo ambalo ni bao lake la 701.
Mbali na Ronaldo aliyefunga bao hilo katika dakika ya 81, mabao mengine ya timu hiyo yalifungwa na Marcus Rashford dakika ya 65 wakati Diogo Dalot ndiye aliyefungua ukurasa wa mabao hayo dakika moja kabla ya timu hizo kwenda mapumziko.
Kwa Ronaldo, mshindi mara tano wa Ballon D’Or, bao hilo linatoa kila dalili ya mwanzo mpya baada ya kupitia kipindi kigumu cha kusakamwa kila kona zaidi kwa kutakiwa aache kujiona kuwa mkubwa kuliko timu kwa kitendo chake cha kususa.
Hata hivyo wakati jina la mchezaji huyo linatajwa kukawa na hali ya sintofahamu miongoni mwa mashabiki baadhi wakishangilia na wengine wakitoa kauli kama za kumpinga mchezaji huyo.
Kwa ujumla Man United sasa itakuwa na kazi moja ya kumalizia na ushindi mechi ya mwisho ya kundi lake dhidi ya Real Sociedad, mechi ambayo itaamua nani awe kinara wa kundi lao ili kuepuka kucheza play-off dhidi ya Juventus, Barcelona au Atletico Madrid ambazo zinahamia Europa Ligi baada ya kukwama kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Wakati Man United ikitamba hali haikuwa nzuri kwa Arsenal ambayo imevurugiwa rekodi yake ya ushindi katika Europa Ligi baada ya kulala kwa mabao 2-0 ugenini mbele ya PSV Eindhoven. Kabla ya mechi ya jana Arsenal ilikuwa imeshinda mechi zake zote nne za Europa na kujikusanyia pointi 12.
Awali Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta alisema kwamba timu yake inatakuwa kuibuka na ushindi ili iwe kinara wa kundi na hivyo kuepuka kucheza dhidi ya timu zitakazokwama kwenye Ligi ya Mabingwa jambo ambalo litakuwa ni kujiongezea ugumu.
“Nimekatishwa tamaa, hatukuwa hata karibu ya ubora wetu na tunajua kwamba Ulaya ni vigumu kushinda, nimeona vijana wakiishiwa nguvu kwa kukimbia kwa sababu tulilazimika kuusaka sana mpira,” alisema Arteta.
PSV ambayo inanolewa na mshambuliaji wa zamani wa Man United, Ruud van Nistelrooy ilitawala vyema mchezo huo ambapo nafasi tatu za mabao walizitumia vyema lakini mwamuzi aliyakataa mabao hayo kwa sababu wachezaji wao waliotea.
Matokeo ya mechi za Europa Ligi…
PSV Eindhoven 2-0 Arsenal
Man Utd 3-0 Sheriff Tiraspol
Zürich 2-1 Bodø/Glimt
AEK Larnaca 3-3 Dynamo Kyiv
Fenerbahçe 3-3 Rennes
Ludogorets 0-1 Real Betis
Union Berlin 1-0 Sporting Braga
Malmö FF 0-2 Union Saint-Gilloise
Lazio 2-1 FC Midtjylland
HJK Helsinki 1-2 Roma
Omonia Nicosia 0-2 Real Sociedad
SK Sturm Graz 1-0 Feyenoord
