Na mwandishi wetu
Mabosi wa klabu ya Azam inadaiwa wanatarajia kukutana leo kumjadili kocha wa timu hiyo, Denis Lavagne raia wa Ufaransa hasa kwa kuwa mwenendo wa timu hiyo si mzuri.
Kocha huyo aliyetua Septemba 6, mwaka huu kurithi mikoba ya Abdihamid Moallin amekuwa na mwendo wa kusuasua baada ya kuiongoza timu hiyo kwenye michezo minne ya Ligi Kuu ya NBC akishinda miwili na kufungwa miwili ukiwemo wa jana aliofungwa na KMC mabao 2-1.
Azan pia ilisukumwa nje ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kufungwa jumla ya mabao 3-2 na Al Akhdar ya Libya kwenye hatua ya pili ya awali ya michuano hiyo.
Taarifa kutoka viunga vya maskani ya timu hiyo, Chamazi, Dar es Salaam vinatanabaisha kuwa hali si shwari kwa kocha huyo na kwamba kwa sasa anakutana na maswali magumu juu ya hatma yake baada ya kushindwa kutoa kilichotarajiwa na mabosi wa timu hiyo.
Alipotafutwa Kaimu Ofisa Habari wa Azam, Hashim Ibwe kulitolea ufafanuzi hilo, alikuwa na majibu machache: “Kweli jana tulipoteza mchezo lakini mpaka sasa hali iko shwari, wachezaji wapo kambini na kocha anafanya juhudi zake kuhakikisha tunafanya vizuri mchezo unaokuja.”
Lavagne aliiongoza Azam kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Mbeya City na kushinda bao 1-0 kabla ya kufungwa na Tanzania Prisons bao 1-0 kisha akaibamiza Singida United kwa bao 1-0 pia kabla ya kuvaana na Akhdar na mwisho kufungwa na KMC.
.
