Na mwandishi
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limemtaja mwamuzi wa kati Ramadhan Kayoko kuwa ndiye atakayeamua mchezo unaosubiriwa kwa hamu wa Yanga dhidi ya Simba utakaounguruma keshokutwa Jumapili.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TFF saa chache zilizopita, Kayoko ambaye ni mwamuzi bora wa Ligi Kuu Bara kwa misimu miwili mfululizo ya 2019-20 na 2020-21 atasaidiwa na Mohamed Mkono na Janeth Balama kama waamuzi wasaidizi.
Aidha, mwamuzi wa akiba katika mechi hiyo itakayopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam atakuwa Elly Sasii na kamisaa wa mechi hiyo ni Kamwanga Tambwe.
Mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu na mashabiki wengi wa soka Afrika Mashariki na Kati kutokana na umaarufu na upinzani uliopo baina ya timu hizo za Kariakoo, Dar es Salaam unakuwa wa pili msimu huu baina yao lakini ni wa kwanza kwa maana ya michuano ya Ligi Kuu.
Timu hizo awali zilikutana kwenye mechi ya Ngao ya Jamii iliyopigwa Agosti 13, mwaka huu na Yanga kuibuka kidedea kwa ushindi wa mabao 2-1. Mabao ya Yanga yaliwekwa kimiani na Fiston Mayele na bao pekee la Simba lilifungwa na Pape Sakho.
Soka Kayoko kupuliza filimbi Yanga, Simba
Kayoko kupuliza filimbi Yanga, Simba
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
