Na mwandishi wetu
Kocha wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 23, Hemed Moroco amesema kuwa kikosi chake kipo kamili na tayari kwa mechi ngumu dhidi ya Nigeria inayotarajia kupigwa kesho kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Kikosi hicho kitaingia kwenye ngwe hiyo nyingine kuwania kushiriki michuano ya Afcon kwa umri huo itakayofanyika nchini Morocco, mwakani baada ya kuiondosha Sudan Kusini kwenye hatua iliyopita kwa sare ya mabao 3-3. Mechi ya kwanza iliyopigwa Dar es Salaam iliisha kwa suluhu na mechi ya pili iliyopigwa Rwanda kama nyumbani kwa Sudan Kusini iliisha kwa sare hiyo na Tanzania kusonga kwa faida ya mabao ya ugenini.
Akizungumza na GreenSport, Kocha Moroco alisema kikosi chake hicho maarufu kwa jina la Ngorongoro Heroes kipo tayari na vizuri kiakili, kimwili ambapo licha ya kufahamu ugumu wa mechi hiyo lakini anaamini kwa maandalizi mazuri waliyokuwa nayo, watapata matokeo.
“Hii ni mechi nyingine inakuja na mbinu nyingine, tumejaribu kurekebisha makosa yaliyoonekana mechi ya kwanza, kwa kuongeza mazuri kwa hiyo naamini tutapata matokeo. Nawashukuru Watanzania kwa kutusapoti na waendelee hivyo, na sisi hatutawaangusha,”alisema.
Nahodha wa Ngorongoro, Ally Msengi naye alisema wanatarajia kukutana na mechi ngumu kutokana na timu za Afrika Magharibi huwa zina nguvu na upambanaji wa hali ya juu lakini kwa mbinu walizopatiwa anaamini watafanya vizuri hiyo kesho.
Baada ya mchezo huo, Ngorongoro itakwenda Nigeria katika mchezo wa marudiano kupata mshindi mmoja atakayesonga mbele hatua inayofuata.
Upande wa Nigeria inayowakilisha kanda ya Afrika Magharibi (WAFU) imeanzia raundi ya pili kufuzu fainali hizo huku mara ya mwisho kushiriki michuano hiyo ikiwa ni mwaka 2019 na kuishia hatua ya makundi. Nigeria pia iliwahi kutwaa ubingwa wa Afcon kwa umri huo mwaka 2015.
Soka Moroco: Tupo sawa kuikabili Nigeria
Moroco: Tupo sawa kuikabili Nigeria
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
