Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa KMC, Thierry Hitimana ameweka wazi kuwa mchezo wao wa keshokutwa dhidi ya Azam utakuwa mgumu kutokana na mazingira ya wapinzani wao kwa sasa.
Hitimana alifunguka kuwa kiwango walichokionesha Azam kwenye mechi yao ya mwisho ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Akhdar licha ya kutolewa kwa kufungwa jumla ya mabao 3-2, kimewashtua.
Pia kocha huyo raia wa Rwanda alisema kingine kinachofanya mchezo huo uwe mgumu zaidi kwao ni hasira za Azam za kutaka kufanya vyema pia msimu huu ili irejee kwenye michuano ya Afrika kwa msimu ujao.
“Leo tumemaliza salama mazoezi na vijana wako tayari kwa mechi lakini ni mechi ambayo itakuwa ngumu mno upande wetu kutokana na kiwango kilichooneshwa na Azam kwenye mechi yao ya mwisho, wangeweza kusonga mbele isipokuwa walikosa tu bahati.
“Lakini pia Azam ni miongoni mwa timu tatu bora Tanzania kwa sasa na ukiangalia wameshatoka Shirikisho hivyo wataelekeza nguvu zao zote kwenye ligi ili wafanye vizuri na msimu ujao warejee kwenye michuano ya kimataifa,” alisema Hitimana.
Pamoja ya kwamba, timu hizo zinafuatana kwenye msimamo wa ligi zikiwa zimepishana kwa pointi moja lakini Hitimana anaamini hiyo pia itachangia kuongeza ugumu wa mchezo maana Azam atapambana asishushwe na KMC.
Azam ambayo itakuwa mgeni kwenye mechi hiyo itakayopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam inashika nafasi ya tano ikiwa na pointi 11 wakati KMC ni ya sita kwa pointi zake 10.
Soka Hitimana aihofia Azam
Hitimana aihofia Azam
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
