Paris, Ufaransa
Nahodha wa timu ya Taifa ya Argentina, Lionel Messi amesema mabingwa watetezi, Ufaransa na Brazil ndizo timu zenye nafasi kubwa ya kutwaa Kombe la Dunia kwa sababu zina wachezaji waliocheza pamoja kwa muda mrefu.
Messi alisema wakati wote Brazil, Ujerumani, Ufaransa, England na Hispania ni timu zinazopewa nafasi ya kubeba taji hilo lakini yeye anaamini Ufaransa na Brazil ndizo timu mbili bora zitakazoingia kwenye fainali hizo zinazotarajia kuanza Qatar, Novemba 20 mwaka huu na kufikia tamati Desemba 18.
“Wakati wote huwa tunazichagua timu zile zile kubwa lakini kama nitachagua kwangu ni Brazil na Ufaransa, hizi ni timu mbili zenye nafasi kubwa ya kushinda taji la dunia,” alisema Messi.
“Wana kundi la wachezaji waliokaa pamoja muda mrefu, wanafanya kazi yao vizuri, timu ya Ufaransa tangu ifanye vibaya na kutolewa kwenye Euro hatua ya 16 bora, wamekuwa na wachezaji wazuri, wamekuwa na mtazamo huo huo na kocha yule yule (Didier Deschamps) na Brazil nayo kwa kiasi fulani ipo hivyo hivyo (chini ya kocha Tite),” alisema Messi.
Katika hali ya kushangaza, Messi hakuitaja Argentina ambayo ina rekodi ya kucheza mechi 35 bila kupoteza hata moja na ndiyo iliyobeba taji la Copa America baada ya kuibwaga Brazil katika hatua ya fainali ingawa timu hiyo hivi karibuni imejikuta ikiandamwa na wachezaji wake muhimu majeruhi, Paulo Dybala na Angel Di Maria.
Kocha wa Argentina, Lionel Scaloni alisema kwamba kwa sasa wachezaji wake wanakabiliwa an wingi wa mechi hasa katika kipindi cha Oktoba lakini akawataka kuangalia mbele.
“Tuko katika kipindi kigumu, wachezaji wanacheza mechi nyingi, kunaweza kuwa na tatizo, kuna kuumia, adhabu, hiyo ni sehemu ya kuwa mchezaji mkubwa, mchezaji wa timu ya taifa, linatia hofu hilo lakini hakuna cha kufanya, naamini wachezaji wataingia uwanjani kucheza si kufikiria kitakachotokea, wacheze kama kawaida yao bila hofu,” alisema Scaloni.
Argentina kwenye fainali za Kombe la Dunia itajitupa uwanjani Novemba 22 katika mechi yake ya kwanza ya Kundi C dhidi ya Saudi Arabia. Timu nyingine katika kundi hilo ni Mexico na Poland.
Kimataifa Messi azipa Brazil, Ufaransa Kombe la Dunia
Messi azipa Brazil, Ufaransa Kombe la Dunia
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
