Na mwandishi wetu
Timu ya soka ya wasichana chini ya miaka 17 ya Tanzania, Serengeti Girls imefuzu kucheza hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na Canada jioni ya leo Jumanne.
Katika mechi iliyopita Serengeti iliishangaza dunia katika michuano hiyo inayoendelea nchini India baada ya kuilaza Ufaransa kwa mabao 2-1 na sasa inajiandaa kucheza na Colombia katika mechi ambayo mshindi atakuwa amejikatia tiketi ya kucheza hatua ya nusu fainali.
Canada ndiyo iliyokuwa ya kwanza kupata bao katika dakika ya 14 lililofungwa na Amanda Allen kwa mkwaju wa penalti lakini Serengeti Girls ilifanikiwa kusawazisha bao hilo dakika 10 kabla ya mapumziko kwa bao lililofungwa na Veronica Mapunda.
Sare ya Serengeti dhidi ya Ufaransa ni moja ya matokeo ya kufurahisha kwa timu hiyo ambayo ilizianza fainali hizo ambazo inashiriki mara ya kwanza kwa kipigo cha mabao 4-0 kutoka kwa Japan na hivyo kuibua hisia kwamba timu hiyo ingekuwa kibonde kwenye kundi lake.
Tanzania imefuzu katika kundi lake pamoja na timu ya Japan na sasa inasubiri kuivaa Colombia katika mechi itakayochezwa Oktoba 22 kwenye Uwanja wa Jawaharlal Nehru Stadium, Margao.
.
Soka Serengeti yatua robo fainali Kombe la Dunia
Serengeti yatua robo fainali Kombe la Dunia
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
