Na mwandishi wetu
Mkurugenzi wa Maendeleo Soka la Vijana Yanga, Mwinyi Zahera amefunguka sababu zilizoifanya Yanga ishindwe kuingia hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika na kuiacha Simba ikisonga mbele kwenye michuano hiyo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Zahera alibainisha kuwa licha ya timu hizo kutoka ligi moja ambayo anaamini haina ushindani wa kutosha kwenye michuano ya Afrika lakini Simba ilikuwa bora zaidi kwenye kuamini kuwa wanapaswa kusonga mbele pamoja na uzoefu wa kucheza mechi za namna hiyo mara kwa mara.
“Unajua Simba wanafanikiwa kwenye fikra sio saikolojia, kichwa chao washakuwa na kujiamini sana kwamba kwenye Ligi ya Mabingwa tunacheza mechi nyingi sana, unapaswa kujiamini kwamba hii ni nafasi yangu nitaenda, Simba wana hicho na kinawasaidia kwenye kujiamini.
“Kwangu mimi naona tumeondolewa na sioni cha kusikitika kwamba tungefanya zaidi ya hapa, tuseme ukweli mechi zote mbili tumecheza na kufanya makosa na kukosa vitu vingi kuendana na kiwango cha mchezo, hakukuwa na mkazo wa mechi kwa mechi zote mbili.
“Lengo la klabu mwaka huu ilikuwa timu iingie makundi, icheze ‘champions league’ lakini ni mpira timu imekutana na mfupa mgumu na ni kujifunza sababu unajua ukiangalia namna gani timu ilijiandaa na namna gani na mechi mbili zilivyochezwa inaonekana kuna vitu vingi vya kujifunza,” alisema Zahera.
Akitolea mfano kwenye mechi yao ya kwanza ya nyumbani dhidi ya Al Hilal ya Sudan iliyoisha kwa sare ya 1-1, mkurugenzi huyo alisema kwamba wachezaji walikosea kwa namna yao uwanjani kama ilivyokuwa kwa benchi la ufundi lilivyochelewa kuwarejesha wachezaji kwenye mipango yao ya mwanzo.
“Mechi ya kwanza tulikosea kipindi cha pili, cha kwanza kulikuwa na nidhamu ya mipango ya kocha, lakini cha pili kukawa na makosa mengi ya uzoefu wa mashindano kwa sababu hutakiwi kuteleza, ukiteleza tu kule utapata shida na utaadhibiwa.
“Sasa baada ya wachezaji kutoka kwenye mipango kipindi cha pili, kulikuwa na mengi yalipasa kufanyika hayakufanyika, wakati wachezaji hawaendi na mipango uwanjani, benchi linapaswa kuja na ufumbuzi wa hilo, niseme kocha alipaswa kuchukua hatua kuleta suluhisho,” alisema.
Zahera hata hivyo alisema bado kuna nafasi ya Yanga kufanya vizuri kwenye Kombe la Shirikisho Afrika walipo sasa endapo watabadilika kimikakati ya mechi na kuwaandaa wachezaji kuwa washindani wanapokutana na wenzao wenye viwango vikubwa hata baada ya kufanya vizuri mfululizo kwenye ligi ya ndani.
Yanga imefungwa jumla ya mabao 2-1 na Al Hilal na kuangukia kwenye Kombe la Shirikisho wakati Simba iliichapa Primeiro de Agosto ya Angola kwa ushindi wa jumla mabao 4-1 na sasa inasubiri kupangwa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Soka Zahera ataja kilichoikwaza Yanga
Zahera ataja kilichoikwaza Yanga
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
