Na mwandishi wetu
Simba imefuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuichapa Primiero de Agosto ya Angola kwa bao 1-0 katika mechi iliyochezwa leo Jumapili kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.
Kwa ushindi huo, Simba inasonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-1 baada ya awali kupata ushindi wa mabao 3-1 katika mechi ya kwanza ambayo Simba ilikuwa ugenini jijini Luanda, Angola.
Alikuwa ni Mosses Phiri aliyeamsha shangwe za mashabiki wa Simba katika dakika ya 33 alipoipatia Simba bao hilo pekee akiitumia vizuri pasi ya Mohamed Hussein Zimbwe Jr.
Katika mechi hiyo Simba ilifanya mabadiliko kadhaa kipindi cha pili ikiwaingiza Habib Kyombo badala ya Augustin Okrah, Gadiel Michael badala ya Zimbwe, Kibu Dennis badala ya Pape Sakho, mabadiliko ambayo hayakubadili matokeo ya mchezo.
Ushindi wa Simba si tu unaipa timu hiyo hadhi katika michuano ya Afrika bali pia kocha wa muda wa timu hiyo, Juma Mgunda naye anazidi kujipa heshima hasa kwa wale ambao walitilia shaka uwezo wake katika michuano mikubwa na yenye hadhi barani Afrika.
Baada ya Simba kufuzu hatua hiyo matumaini mengine ya Tanzania sasa yanabaki kwa timu ya Yanga ambayo leo usiku itakuwa kibaruani nchini Sudan dhidi ya Al Hilal baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na timu hiyo katika mechi ya awali ambayo Yanga ilikuwa nyumbani.
Timu nyingine ambazo tayari zimefuzu hatua ya makundi ya michuano hiyo na kuungana na Simba ni pamoja na Al Ahly na Zamalek za Misri, Memelodi Sundown, Petro Atletico, El Merreikh, Vipers, Raja Casablanca na Al-Ahly Tripoli.
Kwa upande wa Kombe la Shirikisho timu za Azam na Kipanga nazo zitakuwa katika viwanja tofauti zikiipeperusha bendera ya Tanzania. Azam imeanza vibaya mechi yake ya kwanza ugenini kwa kulala kwa mabao 3-0 na hivyo leo itakuwa nyumbani wakati Kipanga ilianza mechi yake nyumbani kwa sare ya bila kufungana dhidi ya klabu ya Club Africain na leo iko ugenini nchini Tunisia.
Kimataifa Simba yatangulia makundi Afrika
Simba yatangulia makundi Afrika
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
